Friday, August 16, 2013

Kanu: Nigeria Itatwaa Kombe la Dunia

Kanu: Nigeria Itatwaa Kombe la Dunia
Nwanko Kanu akiwa pamoja na familia yake.
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa zamani wa Nigeria, Nwankwo Kanu (37), amewatabiria mafanikio makubwa mabingwa wa Afrika, Super Eagles, kwamba wanaweza kuibeba Afrika katika kipute cha fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Brazil.
Nwanko aliyewahi kuchezea kwa mafanikio makubwa katika klabu mbalimbali barani Ulaya ikiwemo Arsenal, amesema kwa ubora wa kikosi cha Super Eagles cha sasa na uwezo wa benchi la ufundi chini Stephen Keshi, timu hiyo itapata mafanikio makubwa katika fainali hizo.
“Tutacheza fainali za Kombe la Dunia mwakani tukiwa na shauku ya kubeba ubingwa kwa niaba ya Afrika. Na kuhusu mechi ya mwisho dhidi ya Malawi, tu tayari na tutashinda,” alisema Kanu alipozungumza na mtandao wa Goal na kuongeza: “Tuna kikosi bora cha ushindani kinachoweza kutupa raha katika fainali za Kombe la Dunia,” alisema Kanu.
“Tunahitaji wachezaji wenye njaa ya mafanikio na wenye uchungu na nchi wenye kutambua wajibu wao katika kuipigania nchi.
“Ndiyo sababu ya timu hii kufanya vizuri, japo uwepo wa nyota wazoefu ni sababu nyingine, wote hupambana kupigania ushindi.
“Nyuma ya wachezaji, tuna benchi lenye makocha bora walio tayari kuipa timu mafanikio,” alisema nyota huyo aliyekuwepo kwenye kikosi cha vijana wa chini ya miaka 23 kilichobeba medali ya dhahabu katika fainali za Olimpiki mwaka 1996.
Hata hivyo, ili Nigeria iweze kuvuka hatua ya makundi na kutinga hatua ya 10 bora itakayotoa timu tano za kwenda Brazil, inakabiliwa na mechi ya mwisho katika kundi F, dhidi ya Malawi itakayochezwa Septemba 6.
Katika mechi hiyo, Nigeria yenye pointi tisa, inahitaji walau sare tu kumaliza kinara wa kundi kutokana na Malawi chini ya Kocha wake Tom Saintfiet kuhitaji ushindi kwani itashuka dimbani
siku hiyo ikiwa na pointi saba.

No comments:

Post a Comment