Tuesday, July 30, 2013

Swaumu yatishia mechi ya Al Ahly, Orlando

Kikosi cha Orlando Pirates
MABINGWA wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Ahly ya Misri wametaka mechi yao ya hatua ya makundi ya michuani hiyo dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyokuwa ipigwe Agosti 4, isogezwe mbele kwa siku tano.
Sababu ya Ahly kuomba hivyo, ni kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hiyo wamalize kwanza funga ya mwezi wa Ramadhani.
“Tumeandika barua kuomba iwe hivyo, lakini tunasubiri jibu kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwamba badala ya kuchezwa Agosti 4, ichezwe Agosti 9,” alisema Mkurugenzi wa Ahly, Sayed Abdel Hafiz.
Alisema wamelazimika kuomba hivyo baada ya wachezaji kugoma kufungulia siku hiyo ya mechi, hivyo hawana la kufanya zaidi ya kuomba ridhaa ya Caf.
“Wachezaji wetu wamekataa kutofunga siku ya mechi hiyo kama ilivyokuwa Jumatano iliyopita tulipocheza na Zamalek,” alisema kiongozi huyo ambaye ameonekana wazi kutoridhishwa na matokeo ya sare.
Pamoja na wachezaji kuruhusiwa kutofunga siku za mechi, jambo hilo limekuwa gumu kutekelezwa na wengi, hivyo kuathiri ufanisi wa timu dimbani.
Aidha, Ahly wamelazimika kusaka uwanja mwingine kwa ajili ya mechi hiyo ya kundi A, baada ya Jeshi la Ulinzi linalomiliki uwanja huo kuuzuia kwa mechi hiyo.
Wiki iliyopita, Ahly walianza kampeni ya hatua ya makundi dhidi ya jirani zao Zamalek katika mechi iliyochezwa mjini El-Gouna, kilometa 450 kutoka Cairo kutokana na sababu za kiusalama.
Kikosi cha Al-Ahly
Licha ya vyombo vya usalama kuruhusu mashabiki 7,000 katika uwanja huo wenye uwezo wa watu 12,000, iliisha kwa amani.
Mamlaka za Cairo wana mpango wa kuipeleka mechi hiyo katika mji wa Aswan, uliopo kilometa 870 kutoka Cairo.
Wakati Zamalek na Ahly zikianza kampeni hiyo kwa sare ya bao 1-1, Pirates walitoka sare ya bila kufungana dhidi ya AC Leopards katika mechi za kwanza katika kundi A.
Timu mbili za juu katika hatua ya makundi, zitaingia katika hatua ya nusu fainali kuwania tiketi ya fainali ambapo bingwa atapata tiketi ya kucheza Klabu Bingwa ya Dunia itakayochezwa Desemba mwaka huu nchini Morocco.

No comments:

Post a Comment