Kazimoto arejea kimiujiza
HATIMAYE kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto, aliyetimkia
nchini Qatar amerejea jijini Dar es Salaam kimya kimya huku uongozi wa klabu yake
ukiwa haufahamu kuhusu ujio wake.
Kazimoto alitoweka bila taarifa akiwa timu ya taifa
‘Taifa Stars’ baada ya kumalizika kwa mchezo wa awali dhidi ya Uganda,
uliomalizika kwa Stars kulala bao 1-0 na nafasi yake kuwa matatani.
Kutokana na kitendo chake hicho, nafasi yake timu ya
taifa ilizibwa na Mudathir Yahya wa Azam FC.
Habari ilizozipata Tanzania Daima jana kutoka kwa mtu wa
karibu na Kazimoto, zilisema kuwa alionekana eneo la Kinondoni Moscow usiku wa
juzi akiwa na baadhi ya wachezaji wa moja ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara
inayomilikiwa na moja ya majeshi ya hapa nchini.
“Mnahangaika kumtafuta na kujiuliza Kazimoto yuko wapi,
mimi nimemuona jana Kinondoni kwa macho yangu akiwa na wachezaji wa ... ila
alikuwa kweli nje ya nchi na amerudi,” alisema mtoa habari huyo.
Aidha, chanzo hicho kilienda mbali na kubainisha kuwa
kiungo huyo ameshindwa kufuzu alikokuwa ndiyo sababu ya kurejea kimya kimya
bila ya kuutaarifu uongozi.
Baada ya kurejea, Kazimoto anatarajiwa kukumbana na
adhabu kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutokana na utovu wa nidhamu
aliouonesha, huku pia klabu yake nayo ikitarajiwa kumpa adhabu pia.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alikaririwa hivi
karibuni kuwa, Kiungo huyo endapo atapatikana atapewa adhabu kutokana na kanuni
ambazo alisaini wakati akiingia kambini zinavyosema.
Kwa upande wa Simba, Katibu wake Mkuu, Evodius Mtawala,
alikiri kusikia taarifa hizo na kudai kuwa wanamsubiri arejee kundini, kwa kuwa
ana mkataba na klabu hiyo.
“Tumesikia tu, ila bado hatujamuona, tunamsubiri akija
mwenyewe klabuni ndipo tutajua jinsi ya kumwadhibu, kwani aliondoka bila ya
kututaarifu,” alisema Mtawala.
No comments:
Post a Comment