Fabregas: Sing’oki Barcelona
BARCELONA waliionya Manchester United chini ya kocha David
Moyes kuwa wanapoteza muda katika jaribio la kumng’oa Cesc Fabregas Nou Camp
kwenda Old Trafford na sasa imedhihirika hivyo.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania, amewaambia marafiki
zake wa karibu kuwa yu tayari kwa vita ya kugombea namba na kujihakikishia
nafasi katika kikosi cha Barca.
Manchester United tayari ilikwishatoa ofa mbili na zote
zikakataliwa na Barcelona, kabla ya sasa kuratibu ofa ya tatu ya pauni milioni
35 ambayo itakuwa rekodi ya klabu.
Fabregas, 26, bado anaongoza orodha ya wakali wanaowindwa na
Moyes kiangazi hiki, lakini chanzo cha ndani klabuni Nou Camp kimethibitisha
juzi usiku: “Cesc amesifia mno ofa za Man United na anatambua nini thamani ya
ofa zao kwake.
“Lakini ni miaka miwili tu tangu alipoondoka England
alikokuwa akiichezea Arsenal na hatarajii kuihama tena Barcelona hususan hivi
karibuni.
“Amekuwa katika vita akijaribu kuchuana na Xavi Hernandez na
Andres Iniesta, ili kufanikiwa kupangwa upande wa pili baada yao, lakini yeye
ameshiriki sehemu ya michezo yao na anahitaji nafasi zaidi ya hiyo,” kilifichua
chanzo hicho.
Na kocha mpya Barca, Tata Martino, ambaye amechukua mikoba
iliyoachwa wazi na Tito Vilanova aliyebwaga manyanga ili kujiuguza kansa ya
tezi, amesisitiza kuwa atomruhusu kijana wake huyo kwenda popote.
Martino alisema: “Man United wanamtaka Cesc? Kama
wamekataliwa ofa zao mbili za kumpata, watambue kuwa nitakataa na ofa yao ya
tatu pia. Cesc atakuwa nasi hapa,” alisisitiza Martino raia wa Argentina.
Fabregas juzi aliripotiwa kuungana na wenzake katika kambi
ya kujiandaa na msimu mpya na alifanyiwa vipimo vya afya kabla ya msimu kisha
kujumuika na wenzake.
No comments:
Post a Comment