Tuesday, July 30, 2013

Klabu Ligi Kuu Bara zaishangaa Yanga
Kikosi cha Yanga SC
SIKU moja baada ya uongozi wa Yanga kugomea haki za Ligi Kuu ya Bara kuhodhiwa na Azam TV, uongozi wa Azam Media wanaomiliki wa televisheni hiyo, umesema kujitoa kwao hakuna athari katika mchakato wa suala hilo ambalo limepokewa kwa furaha na klabu nyinmgine za ligi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa jana na kiongozi wa Azam TV, Said Mohamed ikiwa ni siku moja tangu uongozi wa Yanga kugomea suala la haki za ligi hiyo kumilikiwa na Azam TV kwa hoja kuwa mchakato huo haukuwa wazi na suala hilo lingefanyika baada ya uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania.
Yanga walikwenda mbali zaidi wakisema wao hawastahili kupata mgao sawa na timu nyingine katika mkataba huo kutokana na kuchangia mapato makubwa tofauti na nyingine katika ligi hiyo, hivyo wanastahili kupata mgawo mkubwa zaidi na kuongeza kurusha mechi kutapunguza mapato.
Chini ya mkataba huo wenye thamani ya sh bil 5.6 kwa kipindi cha miaka mitatu, kila klabu itapata kiasi cha sh mil 25 kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 24 na baada ya kwisha kwa ligi hiyo, kila moja itapata sh mil 75.
Akizungumzia tamkoa la Yanga, Mohamed alisema kujitoa kwa Yanga katika suala hilo, hakutaaathiri mchakato wake wakiamini udhamini huo ni wenye tija kwa klabu za Ligi Kuu ambazo zimekuwa zikilemewa na gharama kubwa za uendeshaji.
Alisema kama Yanga watajitoa, hawataathiri uwepo wa udhami huo kwani watakachofanya ni kurusha mechi 13 za ugenini za timu hiyo na kuachana na mechi za nyumbani ambazo watakuwa na haki nazo kisheria.
“Kama kweli Yanga wataamua kujitoa, haina shida…. hatuwezi kuwalazimisha. Tutakachofanya ni kutorusha mechi ambazo wao watakuwa nyumbani, lakini zile za ugenini zitarushwa kama kawaida kwa mfano Shooting vs Yanga,” alisema Mohamed na kusema anaamini mpango huo ni ukombozi kwa kwa timu nyingine za ligi hiyo na kuongeza:
“Ligi Kuu ina timu 14….kama Yanga wataamua kujiweka kando na mkataba huo, bado hakutaathiri kitu maadamu klabu nyingine ni ukombozi mkubwa kwao, hivyo tutakuwa hatuzitendei haki nyingine ambazo kwa miaka mingi timu zimekuwa zikilemewa na mzigo
wa uendeshaji,” alisisitiza.
Wakati Yanga wakipinga udhamini huo, uchunguzi wa Gazeti hili umebaini kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu zimeupokea kwa mikono
miwili kwa hoja kuwa walau sasa zitapunguza matatizo kwa kwani kiasi cha sh mil 100, nje ya nauli na vifaa kutoka kwa mdhamini
mkuu wa ligi hiyo, kampuni ya Vodacom, kutazipunguzia klabu makali ya ukata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa klabu za Coastal Union, Ashant United na Ruvushooting, wametamka wazi kuwa mkataba huo ni ukombozi mkubwa sio kwao tu, bali kwa klabu zote za Ligi Kuu na soka
ya Tanzania na kwenda mbali zaidi wakisema Yanga wana agenda yao binafsi.
Katibu Mkuu wa Ashant United iliyopanda daraja msimu huu, Abubakar Silas alisema kiasi cha sh mil 100 kwa kila klabu kwa msimu, ni ukombozi mkubwa kwa klabu kwani zitawasaidia kufanya mambo yao bila ya ubabaishaji, hivyo kuongeza hata ushindani wa soka uwanjani kutokana na ukweli kuwa ukata kuchangia timu kufanya vibaya.
“Ukweli ni kuwa, Azam TV ni mkombozi wa soka la Tanzania. Naamini kwa udhamini huu, kwetu Ashant Utd tutafanya mambo makubwa katika ligi kwani haijawahi kutokea kila timu ikapata kiasi hicho cha fedha, umefika wakati sasa watu wakubali mabadiliko kama kweli tunataka kupiga hatua,” alisema Silas.
Naye Ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema hofu kubwa ya Yanga, ni kuhofia changamoto kisoka kwani kila timu sasa itakuwa fti kifedha tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo kwa kiasi kikubwa timu kubwa zilikuwa na ufanuu mkubwa kupitia mapato ya milangoni na udhamini binafsi.
“Kitendo cha Azam TV kudhamini Ligi Kuuu ni jambo la kupongezwa badala ya kukatishwa tamaa, hawa Yanga wanaonekana wana agenda yao ambayo haina nia njema na maendeleo ya soka ya Tanzania, kwani hoja zao hazina mashiko.
Naye Ofisa Habari wa Coastal Union, Edo Kumwembe alisema wamepokea udhamini huo wa kihistoria ambao haujawahi kutokea katika soka ya Tanzania na kuongeza kuwa kama watu wataweka kando unafiki na kuzungumza ukweli, hata kama ungekuwa wa thamani ya sh mil 50, bado ni wenye tija kwa klabu nyingi katika ligi hiyo.
“Tena huu ni mwanzo…hapo baadae tunaweza kukaa kuuboresha zaidi, jamani kuna timu ambazo zimekuwa zikisajili kwa shida, achilia mbali sisi wenye udhamini wa Binslum, kuna timu zina ukata mkubwa, inaonekana wazi Yanga hawa wana jambo,” alisema Kumbwembe.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema hawawezi kutoa kauli yoyote juu ya uamuzi wa Yanga kwani bado halijafikishwa kwao kimaandishi, lakini alionesha kushngazwa na kali kuwa Yanga haikushirishwa kwenye mchakato wa jambo hilo.
“Hatujapokea barua ya Yanga, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo baada ya kuona msingi wa madai. Lakini kwa hoja kuwa hawakuwa na mwakilishi, si kweli Katibu Mkuu Mwalusako (Laurance) na Makamu Mwenyekiti  Sanga (Clement) wameshiriki kubariki maamuzi ,” alisema Wambura.
Kuhusu hoja kwanini jambo hilo lisifanyike baada ya uchaguzi mkuu, Wambura alisema TFF iliamua kugawa majukumu yaliyowapa nguvu Kamati ya Ligi kukaa mezani kujadili udhamini huo chini ya dhama ya mgawanyo wa majukumu ambapo si Shirikisho hilo kufanya kila kitu.

No comments:

Post a Comment