MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England umeanza vibaya kwa timu ya Arsenal ambayo ikicheza nyumbani ilikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Aston Villa.
Arsenal wakicheza mbele ya mashabiki 60,003, walionekana kushindwa kuhimili kishindo cha wageni Aston Villa, licha ya kutangulia kupata bao dakika ya sita likifungwa na Olivier Giroud.
Hata hivyo Aston Villa walicharuka na kusawazisha bao hilo dakika ya 22, likifungwa na Christian Benteke, hivyo kwenda mapumziko matokeo yakiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha mashambulizi kwa pande zote mbili na dakika ya 61, Benteke aliifungia bao la pili Aston Villa kabla ya Antonio Luna kufunga la tatu, hivyo kuondoka na ushindi wa mabao 3-1.
Katika mechi nyingine ya mapema, Liverpool wakicheza kwenye Uwanja wao wa Anfield, waliianza ligi kwa furaha baada ya kuvuna ushindi wa bao 1-0, likifungwa na Daniel Sturridge.
Nayo West Ham United ilishinda 2-0 dhidi ya Cardiff na Sunderland ikichapwa bao 1-0 na Fulham huku Norwich City ikitoka sare ya 2-2 na Everton.
Aidha, timu ya West Bromwich Albion ikicheza nyumbani, ilianza msimu kwa kipigo cha bao 1-0m kutoka kwa Southampton.
Ligi hiyo inayoshindanisha timu 20, itaendelea tena kesho kwa miamba ya ligi hiyo kuendelea kutupa karata za kwanza kwa wageni Crystal Palace kuwaalika Tottenham huku Chelsea wakiwa wenyeji wa Hull City.
Manchesster City wao watasubiri hadi kesho kuwakaribisha Newcastle United.
No comments:
Post a Comment