Saturday, July 20, 2013

Mourinho na Terry
Mourinho amtisha Terry
NAHODHA wa Chelsea, John Terry ana kibarua kigumu cha kupigania majaaliwa yake klabuni Stamford Bridge.
Kocha mpya wa mabingwa hao wa Europa League, Jose Mourinho amemwambia nyota huyo muhimu na kiongozi wa kweli dimbani kuwa anapaswa kuthibitisha ubora wake kikosini.
Mourinho alisema: “Terry hayuko salama na mwenyewe analitambua hilo. Jambo pekee ambalo anajua liko salama ni urafiki wetu na mahusiano yetu.
“Tumezungumza kuhusu hilo na kimsingi anatambua kwa ukamilifu kabisa kwamba urafiki ni urafiki na biashara baina yetu ni jambo jingine kabisa. Hii ni biashara hivyo, ndiyo, yeye anatakiwa kuboresha kiwango na uwajibikaji wake.
“Mimi kamwe siwezi kumlinda wala kumpa upendeleo kikosini mbele ya mwingine yeyote – na analitambua hilo kwa sababu anajua asili yangu,” alisisitiza Mourinho aliyeihama Real Madrid na kurejea Chelsea.
Terry, 32, ni beki wa kati aliyebakisha miezi 12 katika mkataba wake wa sasa na klabu hiyo na Mourinho anamtaka kukabiliana vema na changamoto kuhakikisha anathibitisha ubora wake ili aweze kuambulia mkataba mpya.
Mreno huyo aliongeza: “Kutokana na muonekano wa kimwili katika ubora, Terry anahitaji kufanya kazi kwa bidii na hapaswi kupata majeruhi kwa sababu majeraha yanavunja mageuzi ya mchezaji yeyote.

“Kwangu mimi, hiyo ndiyo hatua ya msingi kwa Terry. Anapaswa kuimarisha na kuthibitisha ubora wake kama mwingine yeyote,” alisema Mourinho kwa msisitizo.

No comments:

Post a Comment