MALINZI aliyekalia kiti hicho baada ya juzi kumshinda mpinzani wake Athumani Nyamlani kwa kura 73 dhidi ya 52, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo, Hamidu Mbwezeleni.
Mbali ya msamaha huo kwa wadau waliofungiwa kujihusisha na soka, Malinzi aliomba idhini ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kuvunja Kamati zote ndani ya Shirikisho hilo na kuziunda mpya ambapo lilipita bila kupigwa na wajumbe kwa kugonga meza.
Aidha, Malinzi aliwashukuru wapiga kura kwa kuonesha imani dhidi yake hadi kumchagua na kuahidi kuwa mkutano mkuu wa Shirikisho hilo utakuwa ukifanyika kwa kuzunguka katika mikoa mbalimbali badala ya kufanyika sehemu moja kika wakati.
“Kama mnavyojua Rais wa TFF ni mhimili mkubwa, hivyo basi nawaomba wajumbe na wadau wote hata wale ambao hamjabahatika kuchaguliwa, tushirikiane bega kwa bega tufanikishe azimio letu,” alisema Malinzi na kuongeza msahama huo hauhusu klabu kutokana na kuwa na taratibu zake.
Aidha, aliisihi sekretariet kuwapa siku moja zaidi wajumbe wa Mkutano Mkuu waweze kuendelea kuwa pamoja katika hotel ya Landmark Ubungo kupata fursa ya kubadilishana mawazo kabla ya kuondoka leo, jambo ambalo pia lilishangiliwa na ukumbi mzima.
Kwa upande wa Makamu wa Rais, Wallace Karia aling’ara kwa kura 67 akimbwaga aliyekuwa mshindani wake mkubwa, Ramadhan Nassib aliyepata kura 52 huku Imani Madega aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga na Chama cha soka Mkoa wa Pwani (Corefa) akiambulia kura sita.
Washindi kwa upande wa Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika Kanda ya Geita na Kagera, ni Kalilo Samson aliyepata kura 96 kati ya 120; Kanda ya Mara na Mwanza, ni Vedastus Lufano aliyevuna kura 51 akimshinda Samweli Nyalla (39), Mugisha Galibona (24) na Jumbe Magati (11).
Mshindi katika Kanda ya Shinyanga na Simiyu, ni Epaphra Swai aliyepata kura 63 dhidi ya 61 za Mbasha Matutu.
Mshindi katika Kanda ya Arusha na Manyara, ni Omar Walii Ali (53), aliyewashinda Elley Mbise (51) na Ali Mtumwa (19) huku Ahmed Mgoyi akitetea nafasi yake katika Kanda ya Kigoma na Tabora kwa kura 92 dhidi ya Yusuf Kitumbo aliyeambulia kura 28.
Kanda ya Katavi na Rukwa, ushindi umekwenda kwa Blassy Kiondo kwa kura 73 akimbwaga Ayubu Nyaulingo aliyepata kura 52 huku Ayoub Nyenzi akishinda kupitia Kanda ya Iringa na Mbeya kwa kura 59, ambaye baada ya kusikia matokeo alipoteza fahamu kwa furaha.
Nyenzi aliibuka mshindi akiwapiku washindani wake Elias Mwanjala (46), John Kiteve (12) na David Lugenge aliyeambulia kura nane.
Kanda ya Njombe na Ruvuma, ushindi ulikwenda kwa James Mhagama kwa kura 93 akimbwaga Stanley Lugenge aliyepata kura 31 na katika Kanda ya Lindi na Mtwara, Athuman Kambi alishinda kwa kura 84, akiwabwaga Francis Ndulane (30) na Zafarani Damoder 11.
Kanda ya Dodoma na Singida, mshindi ni Hussein Mwamba kwa kura 63, akiwashinda Stewart Masima (58) na Charles Komba aliyeambulia kura nne.
Geofrey Nyange ‘Kabulu’ alishinda kwa Kanda ya Morogoro na Pwani kwa kura 78, akimshinda Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Njoki aliyepata kura mbili pekee.
Mshindi kuwakilisha Kanda ya Kilimanjaro, ni Khalid Mohamed kwa kura 69 akimshinda Davis Mosha aliyepata kura 54 huku mshindi wa Kanda ya Dar es Salaam, ni Wilfred Kidau aliyepata kura 60, akimshinda Said Balhabou (50), Omary Isaac (10) na Alex Crispine (4).
Rais Leodegar Chilla Tenga aliyemaliza muda wake baada ya kuliongoza Shirikisho hilo tangu Desemba 27, 2004, alimpongeza Malinzi kwa ushindi na kuahidi kutoa ushirikiano huku akimkabidhi katiba ya Shirikisho hilo na mpira, japo makabidhiano rasmi yatafanyika Jumamosi ya wiki hii.
No comments:
Post a Comment