Saturday, September 14, 2013

Simba yatafuna Dar, Yanga chupuchupu

Simba yatafuna Dar, Yanga chupuchupu
Mashabiki wa Simba wakiwa wenye furaha

KWA mara katika Uwanja wa nyumbani wa Taifa, jijini Dar es Salaam tangu kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 24, Simba jana walivuna ushindi wa bao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro.
Katika mechi hiyo, Simba walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi kali katika dakika ya 13, lakini nyota wake Vincent Barnabas, alishindwa kuipatia timu yake bao.
Dakika ya 18, Salim Abdallah wa Mtibwa Sugar alilimwa kadi ya njano na dakika ya 30, Shaaban Kisiga wa Mtibwa Sugar alishindwa kuitendea haki krosi ya Hassan Ramadhani aliyewalamba chenga mabeki wa Simba.
Dakika ya 40, Masoud Mohamed wa Mtibwa Sugar, alilimwa kadi ya njano kwa kucheza vibaya na hadi mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma anamaliza kipindi cha kwanza, kulikuwa hakuna bao.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa kila moja kutaka kupata bao na dakika ya 67, Simba walipata bao likifungwa na mtoke benchi, Henry Joseph Shindika aliyerejea Msimbazi msimu huu baada ya kumaliza mkataba wake nchini Norway.
Shindika alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha pasi ya Haruna Chanongo iliyotokana na kona ndogo, hivyo kuongeza kasi ya mchezo huo.
Bao hilo lilifungwa wakati ambao Mtibwa Sugar wakionekana kucheza soka ya kutulia zaidi wakimpa wakati mgumu kipa Dhaira, aliyefanya kazi kubwa ya kuokoa michomo ya nyota wa Mtibwa Sugar, mabingwa mara mbili wa Ligi Kuu, mwaka 1999 na 2000.
Dakika ya 72, Dhaira alilimwa kadi ya njano kwa kupoteza muda kwa makusudi.
Dakika ya 90, Simba walipata bao la pili likiwekwa wavuni na mtokea benchi, Betram Mwombeki, ikiwa ni dakika tano tangu alimwe kadi ya njano kwa kumchezea vibaya beki wa Mtibwa Sugar chini ya kocha wake Mecky Maxime, nahodha wa zamani wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba chini ya kocha wake Abdallah ‘King’ Kibadeni Mputa na Jamhuri Kihwelo Julio, wamefikisha point na Jamhuri Kihwelo Julio, wamefikisha pointi saba, wakishinda mechi mbili na sare moja.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Masoud Chollo, Issa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas
Mkude, Twaha Ibrahim, Said Hamis, Amis Tambwe, Amri Kiemba na Haruna Chanongo.
Mtibwa Mtibwa: Hussein Shariff, Hassan Ramadhan, Paul George, Dickson Mbeikya, Salim Abdalla, Shaban Nditi, Ally Shomari, Soud Mohamed, Juma Liuziog, Shaaban Kisiga na Vincent Branabas.
Jijini Mbeya, Mbeya City jana walivuna sare ya bao 1-1 dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga katika mechi kali ambayo mabingwa watetezi, Yanga, walifanya kazi ya ziada kuepuka kichapo.
Mbeya City walianza kufika langoni mwa Yanga dakika ya kwanza tu kwa shambulizi kali na Yanga wakijibu dakika ya tano.
Wenyeji walirejea mara ya pili kwenye lango la Yanga dakika ya sita, wakifanya mashambulizi mawili, lakini mabeki wa Yanga wakiongozwa na Nadir Harob Cannavaro, walifanya kazi kubwa.
Yanga walifanya shambulizi jingine dakika ya tisa baada ya Said Bahanuz kupata nafasi nzuri, hata hivyo shuti yake ikipaa juu ya lango la Mbeya City.
Dakika ya 11, shuti ya Steven Mazanda wa Mbeya City ilipaa juu ya lango la Yanga
na dakika ya 16, Mbeya City walipata kona baada ya Cannavaro kuutoa mpira nje.
Dakika ya 17, Mbeya City tena walifanya shambulizi kali, lakini Deus Kisika aliyekuwa mwiba kwa Yanga, alishindwa kuifunga kutokana na kazi kubwa ya mabeki wa Yanga.
Yanga walipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga dakika ya 25, lakini Nizar Khalfan alishindwa na dakika ya 36, Mbeya City nao walikosa bao baada ya shuti ya Anton Matogoro kwenda nje.
Dakika ya 38, Deus Kisika na Steven Mazanda wa Mbeya City walionana vizuri, lakini tatizo likawa umaliziaji.
Dakika ya 44, Mbuyu Twite wa Yanga, alilimwa kadi ya njano kutokana na mchezo mbaya.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa cha ushindani mkali huku Mbeya City chini ya kocha wake Juma Mwambusi wakicheza soka murua na kutangulia kupata bao dakika ya 49, likifungwa kwa kichwa na Mwagano Yeya akiitendea haki pasi ya Hassan wasapili.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo huo kwa Yanga kuongeza nguvu zaidi, lakini Jerry Tegete akishindwa kufunga dakika za 63 na 66 kabla ya Mwagane Yeya wa Mbeya City naye kushindwa kuifungia timu yake dakika ya 67.
Dakika ya 70, Yanga walisawazisha bao likifungwa na Tegete, mtoto wa Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba wa Mwanza, John Tegete, akisawazisha makosa yake ya kushindwa kuzitumia nafasi mbili.
Licha ya timu hizo kupambana kupata bao la uongozi, milango bado iliendelea kuwa migumu huku wenyeji Mbeya City wakionesha uhai mkubwa kiasi cha kulifanya lango la Yanga liwe kwenye msukosuko mkubwa hadi filimbi ya mwisho.
Kwa matokeo hayo, Yanga wamefikisha pointi tano, baada ya kushinda mechi moja na sare mbili kama wenyeji wao Mbeya City, waliopanda msimu huu pamoja na Ashanti Utd ya Ilala na Rhino Rangers ya Tabora
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, mayai matatu yaliokotwa katikati ya uwanja na Meneja wa Uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine, Modestus Mwaluka baada ya kupewa taarifa na waamuzi waliokuwa wakipasha.
Tukio jingine kabla ya kuanza kwa mechi hiyo, ni gari iliyokuwa imebeba wachezaji wa Yanga, kupopolewa mawe wakati inaingia uwanjani hapo na mashabaki wanaodhaniwa ni Mbeya City huku dereva wake akipata jeraha.
Mbeya City: David Burhani, John Kabanda, Hassan Mwasapili, Deogratius Julius, Anton Matogoro, Yohana Morris, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Deus Kisika, Yusuph Wilson/Alex Sett.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez,’ Mbuyu Twite. David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro,’ Kelvin Yondani, Athuman Idd ‘Chuji,’ Nazar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hussein Javu na Said Bahanuzi.
Nayo Ashanti United ya Ilala, imeendelea kuwa gunia la mazoezi kwenye ligi hiyo baada ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja
wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam. Ashant imecheza mechi tatu na kungwa zote.
Katika Uwanja wa Mlandizi, Kibaha, Pwani, Ruvu Shooting pia ya Pwani, walichanua kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wenzao, Mgambo JKT ya Tanga.
Coastal Union ya Tanga nayo jana ilivuna pointi moja baada ya kutoka sare ya bila kufungana na Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Kutoka Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera, Kagera Sugar walivuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam huku bao la wenyeji likifungwa na Felix Themi Hamis Mcha akifunga kwa upande wa Azam.
Katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, JKT Oljoro walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Rhino Rangers ya Tabora, moja ya timu ngeni katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Friday, September 13, 2013

Sturridge, Rodgers watwaa tuzo ya mwezi

Sturridge, Rodgers watwaa tuzo ya mwezi
Sturridge (kushoto), na Kocha Rodgers wakiwa kwa pamoja wameshikilia Tuzo. 
MSHAMBULIAJI wa Liverpool, Daniel Sturridge na Kocha wake Brendan Rodgers wamefanikiwa kupata tuzo ya Mchezaji Bora na Kocha Bora wa Mwezi Agosti katika Ligi Kuu England.
Tuzo hizo wamepata baada ya kushinda kwenye mechi zao zote tatu mfululizo za Ligi hiyo.

Lionel Messi ataka taji la Dunia Brazil

Lionel Messi ataka taji la Dunia Brazil
MSHAMBULIAJI Lionel Messi amesema baada ya kupata mafanikio makubwa kwa ngazi ya klabu akiwa na Barcelona, kilichobaki ni kung’ara akiwa na Argentina kwa kubeba taji la Dunia mwakani.
Messi, nyota bora mara nne wa dunia, amesema ndoto yake kubwa sasa ni kuiwezesha Argentina kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia, mwakani nchini Brazil.
Kauli ya Messi imekuja iku chache tu tangu Argentina chini ya kocha wake Alejandro Sabella, kuvuna ushindi wa mabao 5-2 na kuzidi kuikaribia tiketi ya Brazil.
Kwa ushindi huo wa kishindo katika mechi ya Jumanne wiki hii, Messi
anaamini Argentina yaweza kutwaa ubingwa kama mwaka 1986, ilipofanya hivyo  ikiongozwana nyota wake mahiri Diego Maradona kwa wakati huo.
"Naota kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia. Kitu kilichobaki kwangu ni kuisaidia Argentina, japo ni safari ndegu," alisema Messi alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuifunga Paraguay.
"Tumepata tulichokuwa tukitafuta, lakini tulipata wakati mgumu kucheza hapa, lakini tunashukuru kwani kitu muhimu ni kupata tiketi haraka iwezekanavyo.
"Tunataka kuendelea kupata ushindi wa aina hii,” alisema huku akikana habari kwamba Barcelona imetaka asichezea mechi zilizosalia katika kupigania tiketi "Sijui lolote kuhusu hilo, mara zote hupenda kucheza katika kikosi cha Argentina," alisema.

Thursday, September 12, 2013

Ozil: Sikuthaminiwa Santiago Bernabeu

Ozil: Sikuthaminiwa Santiago Bernabeu
MCHEZAJI Mesut Ozil, amekana kauli ya Rais wa Klabu ya Real Madrid, Florentino Perez, kwamba ameondoka kutokana na kukosa vigezo za nyota wa kimataifa.
Mbali ya kukana hilo, Ozil amesema kilichomwondoa ni kukerwa na kutopewa heshima yake Real Madrid licha ya kuwa katika kiwango bora kiuchezaji.
Ozil ameyasema hayo wakati baba yake mzazi akiwa kwenye harakati za kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Perez kwa kauli yake dhidi ya mwanaye.
Kwa mujibu wa Peres, Ozil alikuwa akitumia muda mwingi kujirusha na wasichana na kukesha kwenye baa.
Hata hivyo, nyota huyo wa kimataifa wa Ujerumani, hakupenda kuingia kwenye vita ya maneno na Perez, akiishia kusema aliondoka kutokana na kutothaminiwa.
"Sitaki kusema lolote baya dhidi ya Real Madrid kwa sababu miaka yangu mitatu pale ilikuwa ya mafanikio.
"Tulibeba mataji na niliisha kwa furaha, kila aliyenifahamu, alitambua mchango wangu kwa Real Madrid.
"Nikiwa pale nilicheza mechi 159, katika mazingira ya kawaida, huwezi kucheza mechi nyingi hivyo kama hupo katika kiwango bora.
"Tatizo sikupata heshima niliyostahili kulingana na mchango wangu. Nilikuwa kwenye mazingira magumu na nilipozungumza kwa simu na Kocha wa Arsenal (Arsene Wenger), alionesha kuniheshimu."
Ozil aliyewahi pia kukipiga Werder Bremen ya Ujerumani, anaamini kutua kwake Arsenal, kutaboresha zaidi kiwango chake.

Bale amuweka kando C.Ronaldo katika utambulisho wa jezi mpya Real Madrid

Bale amuweka kando C.Ronaldo kwenye utambulisho wa jezi mpya Real Madrid



TFF yatoa vibali kwa nyota wa Tanzania

TFF yatoa vibali kwa nyota wa Tanzania

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa nyota wawili wa Tanzania kucheza soka chini Afrika Kusini.
Nyota hao ni Robert Kobelo na Mohamed Ibrahim wamepewa hati hizo baada ya kuombewa na Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kama wachezaji wa ridhaa ili wajiunge na klabu ya Cacau United ambayo timu yake inacheza Ligi Daraja la Pili katika Wilaya ya Cacau.
Naye mchezaji Said Maulid aliyejiunga na Ashanti United akitokea nchini Angola msimu huu amepata ITC ambayo sasa inamwezesha kuchezea timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoingia mzunguko wake wa tatu kesho.

Ozil aanza rasmi mazoezi Arsenal

Mesut Ozil aanza rasmi mazoezi Arsenal
MCHEZAJI mpya wa Arsenal, Mesut Ozil ameyaanza maisha mapya ya Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe akitokea Klabu ya Real Madrid.
Ozil ameoneka akiwa katika mazoezi ya pamoja na wachezaji wenzake wa Arsenal kwenye uwanja mazoezi.
Kiungo huyo ambye ameweka rekodi ya usajili wa bei ghali ya paundi milioni £42.5 (sawa na fedha za Kitanzania bilioni 108. 5