Thursday, August 29, 2013

Yanga SC yashikwa, Mnyama aua

Yanga SC yashikwa, Mnyama aua
Abdi Banda kati kati akiwatoka wachezaji wa Yanga.
 Jerry Santo akipiga penati iliyozaa goli dakika ya 90.
MABINGWA watetezi wa Lgi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC jana walilazimishwa sare ya bao 1-1 na Coastal Union ya Tanga katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Yanga walipata bao dakika ya 68, na Mshambuliaji wao hatari Didier Kavumbagu baada ya kupokea krosi safi iliyopigwa na David Luhende.
Hivyo, Coastal Union walisawazisha dakika ya 90 kwa mkwaju wa penalti iliyofungwa na Jerry Santo, baada ya Luhende kuunawa mpira ndani ya kumi na nane.
Hivyo kila timu ikanyakua pointi moja, na kufikisha pointi nne kila mmoja katika.
Baada ya mechi kumalizika, polisi waliamua kuwatawanya mashabiki wa Yanga kwa kutumia mabomu ya machozi, kutokana na kufanya fujo kwa kukerwa na uchezeshaji wa mwamuzi.
Wale watani wao wa Jadi, Simba ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 kutoka kwa JKT Oljoro.
Nayo Ashanti United jana imeendelea kuwa mdebwedo baada ya kuchapwa bao 1-0 na JKT Mgambo.
Bao pekee la Mgambo JKT walioanza ligi hiyo kwa kichapo kutoka kwa JKT Ruvu, lilifungwa dakika ya 62 na mtokea benchi, Fully Maganga.
Ni kipigo cha pili vijana hao wa Ilalala, Dar es Salaam wakitoka kulimwa mabao 5-1 na mabingwa watetezi, Yanga.

Matokeo mengine
Mbeya City 2-1 Ruvu Shooting
Mtibwa Sugar 1-0 Kagera Sugar
Azam 2-0 Ryno Rengers
JKT Ruvu 3-0 Prisons

Tuesday, August 27, 2013

Mourinho ampa Wayne Rooney saa 48 kuamua

Mourinho ampa Rooney saa 48 kuamua
 
 
 
MRENO Jose Mourinho amempa Wayne Rooney muda wa saa 48 awe ametoa jibu ramsi kama atahama Old Trafford na kwenda Stamford Bridge ama vipi.
Mourinho ameamua hivyo, licha ya kocha wa Man Utd, David Moyes kuwahi kutamka bayana kuwa hayuko tayari kumtoa nyota huyo kwa bei yoyote.
Aidha, Mourinho amesisitiza hilo siku moja tu tangu timu hizo zivune sare ya bila kufungana katika mechi ya Ligi Kuu, ikiwa ya pili kwa kila timu tangu kuanza kwa ligi hiyo Agosti 17.
Hayo yote kutokana na Rooney kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mechi hiyo.
Aidha, Mourinho amemwaga sumu hiyo wakati ambao Rooney (27), akionesha wazi kuwa
anataka kuondoka kutokana na mazingira halisi ya Old Trafford kwa sasa juu ya nafasi yake kwenye kikosi chini ya Moyes.
"Kwa namna moja au nyingine, aseme kama anataka kubaki au kuondoka," alisema Mourinho aliyerejea Stamford Bridge msimu huu akitokea Santiago Bernabeu.
Tangu Rooney atue Old Trafford mwaka 2002 akitokea Everton, ameifungia Manchester United jumla ya mabao 156, hivyo kuwa miongoni mwa nyota muhimu katika safu ya ushambuliaji.
Alipoulizwa kuhusu nyota wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto’o wa klabu ya Anzhi Makhachkala, alisema hilo pia litajulikana baada ya masaa 48.
"Kwa kocha kama mimi, klabu kama Chelsea na watu wafanyai kazi pamoja nami, hatutaki kupoteza muda kwa mchezaji wa klabu asiyotaka kumuuza,” alisema Mourinho aliyewahi kuipa Chelsea ubingwa wa Ligi Kuu.

Euro mil 100 zamng'oa Bale

Euro mil 100 zamng'oa Bale

KLABU ya Real Madrid na Tottenham zimeafikiana juu ya nyota wa kimataifa wa Wales, Gareth Bale aende Santiago Bernaneu kwa kitita cha euro mil 100.
Kiasi hicho kinazidi kile kilichotolewa na klabu hiyo mwaka 2009 kwa Cristiano Ronaldo kumng’oa Old Trafford kwa euro mil 93.
Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, alisema juzi mpango huo umefanikiwa baada ya majadiliano ya kina baina ya klabu hizo mbili.
Japo Real Madrid ilikuwa bado haijapata uhakika wa nyota huyo, Alhamisi iliyopita mashabiki wa Santiago Bernabeu walikuwa na fulana zenye jina la Bale na11.
Kuna habari kuwa, tayari klabu hiyo imeanza kujenga jukwaa rasmi ambalo litatumika kwa utambulisho wa mchezaji huyo kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Habari zinasema licha ya klabu hiyo kufanya maandalizi ya utambulisho wa Bale, yaelezwa presha yake haiwezi kulinganishwa na yale ya Cristiano Ronaldo, Kaka au  Karim Benzema.

Monday, August 26, 2013

KUELEKEA MECHI YA MAN UTD NA CHELSEA LEO Moyes na Mourinho waogopana

KUELEKEA MECHI YA MAN UTD NA CHELSEA LEO
Moyes na Mourinho waogopana
KLABU za Manchesater United na Chelsea zimejikuta katika wakati mgumu kutokana na kila moja kujikuta ikihakikisha inafanya kila liwezalo kukwepa kupokea kipigo kutoka kwa mwenzake.
Klabu hizo ambazo zinatarajiwa kukutana leo katika mchezo wa ligi kuu huku United ikiwa na historia ya kushinda mara mbili na Chelsea mara tatu hali inayoonesha kwamba kila moja ina nafasi ya kushinda mchezo huo lakini kama leo mmoja wao atafanikiwa kuichapa nyingine atakuwa ameandika historia isiyosahaulika.
Iwapo Chelsea watakubali kupokea kipigo kutoka kwa United, itawapa wakati mgumu katika mchezo wao wa Super cup utakao wakutanisha na wababe kutoka Ujerumani klabu ya Bayern Munich.
Mshindi wa mchezo huo kati ya klabu ya Man Utd na Chelsea utachangia kuiwezesha klabu husika kuitangaza na kuiweka katika nafasi nzuri kwenye msimu huu mpya wa Ligi Kuu England.
Kwa upande wa David Moyes anatakiwa kushindwa mechi hii kutokana na ukweli kwamba ni kocha mpya kukutana na Chelsea akiwa na Man United, kwani kwake ushindi ndicho kitu anachokihitaji huku akikwepa pia kupokea kipigo kutoka kwa Chelsea.
Mchezo huo unaonekana kujaa na msisimko kutokana na kwamba wakati Moyes alipokuwa kocha wa Everton klabu ya Chelsea imewahi kumchakaza, hivyo anahitaji kujenga heshima mpya ndani ya Old Trafford.
Klabu zote zinaonesha kujiimarisha katika ushambuliaji na ukuta usiopitika kirahisi hivyo mechi hiyo inategemewa kuwa kali na nzuri!

Man City wachapwa 3-2 na Cardiff

Man City wachapwa 3-2 na Cardiff
MABAO mawili ya vichwa yaliyofungwa na Fraizer Campbell na lingine kutoka kwa Aron Gunnarsson yalitosha kuipatia ushindi wa kwanza Cardiff City tangu wapande daraja la Ligi Kuu England.
Huku mabao mawili ya kupoza moyo yakitiwa kambani na Edin Dzeko pamoja na Alvaro Negredo.
Angalia mabao yalivyofungwa

Thiago Alcantara aumia Bayern ikiua 3

Thiago Alcantara aumia Bayern ikiua 3

BAYERN wamepata pigo baada ya kiungo wake wa kimataifa wa Hispania, Thiago Alcantara kuumia misuli ya katika kifundo cha mguu, hivyo atalazimika kuwa nje ya dimba kwa wiki saba.
Majeraha hayo aliyapata juzi wakati Timu yake ya Bayern ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Nurnberg katika mechi ya Bundesliga iliyochezwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena, mjini Munich.
Katika mechi hiyo, Franck Ribery alifunga bao la kwanza katika dakika ya 69 kabla ya Arjen Robben kufunga jingine huku David Alaba akikosa penalti katika dakika za awali katika mechi hiyo.
Kwa ushindi huo, Bayern sasa wamefikisha pointi tisa, baada ya kushinda mechi zote tatu tangu kuanza kwa msimu.

Sunday, August 25, 2013

Yanga yafungua msimu kwa
mbwembwe, Simba manjanga
Kikosi cha Yanga kikiwa katika pozi la pamoja
Wachezaji wa Yanga wakipongeza baada ya ushindi wa mabao
 5-1. (Picha zote kwa hisani ya HABARI MSETO BLOG)
YANGA, jana iliuanza kwa kishindo msimu mpya kwa kuwatandika Ashanti United ya Ilala mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Slaam huku Simba akivuna sare ya 2-2 na Rhino ya Tabora, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Vijana wa Ernie Brandts, walipata bao la kwanza dakika ya 11, likifungwa na Jerry Tegete akimchambua kipa wa Ashanti United kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Simon Msuva
aliyetoa pasi kwa mfungaji.
Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa Yanga kutaka kuongeza huku Ashanti United chini ya Kocha wake Mbaraka Hassan ikipambana vilivyo kusawazisha, lakini hadi mapumziko mabingwa watetezi, Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Ndani ya dakika hizo 45 za kwanza, kama si wachezaji kadhaa wa Yanga kucheza kwa staili ya kuremba, wangeweza kwenda mapumziko wakiwa na mabao zaidi kutokana na kumiliki mchezo kwa kiasi kikubwa.
Kikwazo cha mabao, kilikuwa ni nyota wa Yanga kushindwa kutumia vizuri nafasi kadhaa walizopata katika dakika ya 40 kwa Haruna Niyonzima licha ya kumchambua kipa Ibrahim Abdallah, akishindwa kufunga kutokana mbwembwe.
Dakika ya 44, Tegete naye alipata nafasi nzuri ya kuweza kufunga baada ya kumzidi mbinu kipa wa Ashanti Utd, lakini akishindwa kuukwamisha mpira katika nyavu huku wapinzani wao wakionekana kupambana na kucheza soka ya kuvutia wakiongozwa na Hussein Sued na Joseph Mahundu.
Tatizo la Asanti United ilikuwa kushindwa kumalizia kwani licha ya kufanya kazi nzuri ya kufika mara kwa mara katika lango la wapinzani wao kiasi cha kufanya kazi kuhimili kishindo cha wageni hao katika Ligi Kuu, mashuti yao yalishindwa kuzifikia nyavu za Yanga
Katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga ilipata pigo baada ya Athumani Idd Chuji kuumia hadi kushindwa kuendelea huku nafasi yake ikitwaliwa na Frank Domayo.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kufanya mashambulizi makali na dakika ya 48, Msuva aliifungia bao la pili kwa shuti kali ya mbali na kumsihinda kipa wa Ashanti Utd, ambaye jana alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo langoni mwake.
Dakika ya 58, Yanga ilipata bao la tatu, likifingwa na Tegete kwa krosi murua ya Msuva ambaye katika mechi ya jana alikuwa mwiba mkali kwa ngome ya Ashanti, ikiwa ni dakika mbili tu tangu beki Ramadhani Malima kufanya kazi kubwa ya kuzuia shuti ya Tegete isiguse nyavu.
Dakika ya 73, Niyonzima alifunga bao la nnne kwa kichwa akiunganisha mpira uliotokana na adhabu ya moja kwa moja uliyopigwa na Luhende na dakika ya 77, beki Emmanuel Kichiba wa Ashanti Utd alitolewa na mwamuzi Oden Mbaga kwa kumchezea vibaya Msuva.
Dakika ya 90, Ashanti United ilipata bao la kufutia machazi, likifungwa na Shaaban Juma kabla ya Nizar Khalfan kuifungia Yanga bao la tano katika dakika za majeruhi, hivyo kuanza ligi hiyo kwa kishindo cha mabao 5-1.
Katika mechi nyingine, Coastal Union ya Tanga, jana walianza vizuri kampeni yao kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Coastal Union, walipata bao la kwanza dakika ya 11, likifungwa na Abdi Banda kwa shuti kali ya umbali wa mita 45 kabla ya Cyprian Odula kufunga la pili dakika ya 34 na kudumu hadi filimbi ya mwisho.
Nayo JKT Ruvu ya Pwani chini ya Kocha wake Mbwana Makata, jana ilianza ligi kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga katika Uwanja wa Mkwakwani, jijini humo katika mechi nyingine ya ufunguzi wa ligi.
Mabao yake kufungwa na Bakari Kondo dakika za 80 baada ya kutokea piga-nikupige langoni mwa Mgambo kabla ya kufunga la pili dakika ya 83, akiwatoka mabeki.
Mbeya City ikicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini Mbeya, ilitoka sare ya 0-0 na Kagera Sugar ya Kagera.
Rhino Rangers ya Tabora, jana ikionja Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, ilifanikiwa kuibana mbavu Simba kwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na kugawana pointi.
Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro, ikicheza kwenye Uwanja wake wa Manungu, ilitoka sare  ya 1-1 na Azam FC, washindi wa pili wa msimu uliopita huku Ruvu Shooting ya Pwani chini ya kocha wake Charles Boniface Mkwasa, ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Mabatini, Kibaha, Pwani.