VITA ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi inaendelea tena usiku wa leo kwa Barcelona kuwakaribisha AC Milan ya Italia katika uwanja wa Camp Nou katika mechi ya kundi H.
Miamba hiyo inakutana ikiwa na kumbukumbu ya sare bao 1-1 katika mechi yao ya Novemba 22 kwenye dimba la San Siro, mali ya mabingwa hao wa Italia wenye rekodi ya kubeba taji la Ulaya mara saba.
Kwa mazingira ya kundi hilo, ni mechi inayotarajiwa kuwa yenye ushindani kwani wakati Bacelona wakisaka ushindi kufikisha pointi 10 kujihakikishia tiketi ya 16 bora, Milan yenye pointi tano nayo inakabiliwa na shinikizo la kushinda mechi hiyo.
Kama Milan itakubali kipigo kutoka kwa Barcelona, kundi hilo litasaliwa na tiketi moja ya 16 bora ambayo itakuwa ikishindaniwa na timu nyingine mbili za Celtic yenye pointi tatu na Ajax yenye pointi moja.
Wakati Barcelona wakitaka kushinda kujihakikishia tiketo, macho na masikio ya mashabiki wa Barcelona vitakuwa kwa Lionel Messi nyota bora mara nne wa Dunia ambaye ameshindwa kuchana vyavu katikamechi nne.
Hiyo inamfanya Messi awe na uchu zaidi wa kufunga kuliko wakati wowote kwani tayari kushindwa kwake kufunga katika mechi hizo zilizopita, kumezua sintofahamu kwa wengi.
Mechi ya mwisho ambayo Messi alishindwa kufunga licha ya kucheza dakika 90, ni ya La Liga iliyochezwa Ijumaa iliyopita kwenye Uwanja wa Camp Nou, ikiwa ya nne ambapo mara ya mwisho kupatwa na ukame kama huo, ni miaka sita iliyopita.
Kwa upande mwingine, Messi aliingia mwezi Oktoba akitokea kuwa majeruhi aliyokuwa amepata Septemba, hivyo aliporejea alishindwa kuziona nyavu dhidi ya Osasuna, Celta Vigo na Real Madrid.
Bao la mwisho nje ya La Liga kwa Messi, ni aliposawazisha dhidi ya AC Milan katika sare ya bao 1-1, likiwa la nne kwake katika michuano hiyo iliyo katika hatua ya makundi na mengine matatu aliyofunga ugenini dhidi ya Ajax.
Ukirejea katika La Liga, katika mechi 10 alizocheza msimu huu, Messi amefunga mabao nane, japo anayo nafasi ya kurejea kwenye makali yake kwani ligi yenyewe ndio kwanza ipo raundi ya 12.
Katika kuhakikisha Messi anarejesha makali yake, nyota wa Barcelona waliowahi kuwa manahodha, wameapa kumsaidia nyota huyo wa kimataifa wa Argentina kama atahitaji msaada wao. Hao ni Xavi, Carles Puyol, Victor Valdes na Andreas Iniesta.
Hata hivyo, Messi mwenyewe amekaririwa na mtandao mmoja wa kijamii wa nchini China wa Weubo akisema bado hajarejea kwenye hali yake ya kawaida kiafya.
"Sipo fiti kwa asilimia 100, lakini naamini nitaanza kurejea kwenye kiwango changu taratibu kwa kadiri nitakavyokuwa nikicheza mechi moja hadi nyingine," alisema.
Naye kocha wa Barca, Gerardo Martino, anayetokea mji mmoja wa Messi wa Rosario, alikana habari kuwa nyota huyo anashindwa kucheza vizuri kutokana na kumhofia, habaria ambazo zilianza baada ya mechi ya Ijumaa iliyopita "Messi haniogopi," alisema. "Ni bahati mbaya tu hakufunga katika mechi kama tatu au nne hivi.”
Kama Messi atabaini tatizo lake, kabla ya Jumatano (leo), mechi ya AC Milan itakuwa mwanzo mpya kwake wa kuanza kufunga.
Wakati Barcelona wanawakaribisha AC Milan wakiongoza La Liga kwa pointi 34, Milan wanashuka dimbani wakiwa nafasi ya 11 Serie A, bada ya kufungwa mabao 2-0 na Fiorentina mechi iliyopita, ikiwa ni mechi ya nne bila ushindi kwake.
Hiyo inamfanya Kocha Massimiliano Allegri kuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki huku yeye akitamka wazi kiwango cha vijana wake katika mechi tatu zilizopita, hakijamridhisha.
Rekodi ya mechi zilizopita kwa miamba hii; Oktoba 22, 2013 AC Milan 1 - FC Barcelona 1; Machi 12, 2013 Barcelona 4 - AC Milan 0; Feb 20, 2013 AC Milan 2 - FC Barcelona 0; April 3, 2012 Barcelona 3 - Milan 1, Machi 28, 2012, AC Milan 0 - FC Barcelona 0.
Chelsea iliyopo kundi E, nayo leo itakuwa na kazi ya kubakisha pointi tatu nyumbani kutoka kwa FC Schalke 04 ya Ujerumani, japo nayo itakuwa ikipigania ushindi kukamata usukani wa kundi kutokana na kushuka dimbani leo ikiwa na pointi sita kama Chelsea.
Mechi nyingine katika kundi hilo, ni Basel ya Uswisi yenye pointi nne iatakayokuwa mwenyeji wa Steaua Bucharest ya Romania yenye pointi moja.
Nayo Arsenal inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya England kwa pointi 25 baada ya mechi 10, leo itakuwa ugenini dhidi ya Borrusia Dortmund ya Ujerumani waliopatia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya msimu uliopita kufungwa na Bayern Munich kwenye fainali, Mei 25.
Wakati Arsenal wakiongoza kundi hilo la F, wakiwa na pointi sita, Dortmund wanafuatia kwa pointi sita kama ilivyo kwa Napoli ya Italia huku Marseille ikiburuza mkia ikiwa mikono mitupu ikichapwa mechi zote tatu.
Katika kundi G, vinara Atletico Madrid ya Hispania wakihitaji walau sare tu kujihakikishia tiketi ya 16 bora kutokana na kuwa na pointi tisa, leo wanawakaribisha kibonde wa kundi hilo, FK Austria Vienna yenye moja.
Mechi nyingine ya kundi hilo, ni kati ya Zenit St Petersburg ya Uswisi iliyo nafasi ya pili kwa pointi nne, iatakayowakaribisha FC Porto ya Ureno, mabingwa wa michuano hiyo wa mwaka 2004.