Tuesday, October 29, 2013

Kim Poulsen amrudisha Mapunda Taifa Stars

Poulsen amrudisha Mapunda Taifa Stars
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 30 wa timu ya pili (Future Young Taifa Stars) kitakachoingia kambini Novemba 9 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Chalenji.
Kipa Ivo Mapunda wa Gor Mahia ya Kenya ni miongoni mwa wachezaji walioitwa na Kim kwenye kikosi hicho ambacho hukitumia kuangalia uwezo wa wachezaji kabla ya kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa.
Kikosi hicho kamili ambacho Novemba 13 kitacheza mechi ya kirafiki na Taifa Stars kinaundwa na; 
Makipa Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya).
Mabeki ni David Luhende (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Himid Mao (Azam), Issa Rashid (Simba), Ismail Gambo (Azam), John Kabanda (Mbeya City), Kessy Khamis (Mtibwa Sugar), Michael Pius (Ruvu Shooting), Miraji Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Said Moradi (Azam) na Waziri Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Farid Mussa (Azam), Haruni Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Khamis Mcha (Azam), Ramadhan Singano (Simba), Simon Msuva (Yanga), William Lucian (Simba).
Washambuliaji ni Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hussein Javu (Yanga), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mwagane Yeya (Mbeya City) na Paul Nonga (Mbeya City).
Kim amesema kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager chenyewe kitaingia kambini Novemba 12 jijini Dar es Salaam ambapo siku inayofuata ndipo kitakapocheza mechi na Future Young Taifa Stars.
Baada ya mechi hiyo, kambi ya Future Young Taifa Stars itavunjwa wakati Taifa Stars itaondoka Novemba 14 mwaka huu kwenda Arusha ambapo itaweka kambi na kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kwenda Nairobi, Kenya kwenye michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu
Wachezaji 16 wa kikosi cha Taifa Stars kitakachoingia kambini Novemba 12 mwaka huu kinaundwa na Ally Mustafa (Yanga), Mwadini Ali (Azam), Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa) na Nadir Haroub (Yanga).
Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam), Mwinyi Kazimoto (Markhiya, Qatar), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC) na John Bocco (Azam).
Wachezaji wengine kumi kutoka Future Young Taifa Stars baadaye wataongezwa katika kikosi kitakachounda timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji.

Monday, October 28, 2013

Malinzi bosi mpya TFF, awatoa wadau kifungoni

Malinzi bosi mpya TFF,awatoa wadau kifungoni
MALINZI aliyekalia kiti hicho baada ya juzi kumshinda mpinzani wake Athumani Nyamlani kwa kura 73 dhidi ya 52, aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho hilo, Hamidu Mbwezeleni.
Mbali ya msamaha huo kwa wadau waliofungiwa kujihusisha na soka, Malinzi aliomba idhini ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kuvunja Kamati zote ndani ya Shirikisho hilo na kuziunda mpya ambapo lilipita bila kupigwa na wajumbe kwa kugonga meza.
Aidha, Malinzi aliwashukuru wapiga kura kwa kuonesha imani dhidi yake hadi kumchagua na kuahidi kuwa mkutano mkuu wa Shirikisho hilo utakuwa ukifanyika kwa kuzunguka katika mikoa mbalimbali badala ya kufanyika sehemu moja kika wakati.
“Kama mnavyojua Rais wa TFF ni mhimili mkubwa, hivyo basi nawaomba wajumbe na wadau wote hata wale ambao hamjabahatika kuchaguliwa, tushirikiane bega kwa bega tufanikishe azimio letu,” alisema Malinzi na kuongeza msahama huo hauhusu klabu kutokana na kuwa na taratibu zake.
Aidha, aliisihi sekretariet kuwapa siku moja zaidi wajumbe wa Mkutano Mkuu waweze kuendelea kuwa pamoja katika hotel ya Landmark Ubungo kupata fursa ya kubadilishana mawazo kabla ya kuondoka leo, jambo ambalo pia lilishangiliwa na ukumbi mzima.
Kwa upande wa Makamu wa Rais, Wallace Karia aling’ara kwa kura 67 akimbwaga aliyekuwa mshindani wake mkubwa, Ramadhan Nassib aliyepata kura 52 huku Imani Madega aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga na Chama cha soka Mkoa wa Pwani (Corefa) akiambulia kura sita.
Washindi kwa upande wa Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika Kanda ya Geita na Kagera, ni Kalilo Samson aliyepata kura 96 kati ya 120; Kanda ya Mara na Mwanza, ni Vedastus Lufano aliyevuna kura 51 akimshinda Samweli Nyalla (39), Mugisha Galibona (24) na Jumbe Magati (11).
Mshindi katika Kanda ya Shinyanga na Simiyu, ni Epaphra Swai aliyepata kura 63 dhidi ya 61 za Mbasha Matutu.
Mshindi katika Kanda ya Arusha na Manyara, ni Omar Walii Ali (53), aliyewashinda Elley Mbise (51) na Ali Mtumwa (19) huku Ahmed Mgoyi akitetea nafasi yake katika Kanda ya Kigoma na Tabora kwa kura 92 dhidi ya Yusuf Kitumbo aliyeambulia kura 28.
Kanda ya Katavi na Rukwa, ushindi umekwenda kwa Blassy Kiondo kwa kura 73 akimbwaga Ayubu Nyaulingo aliyepata kura 52 huku Ayoub Nyenzi akishinda kupitia Kanda ya Iringa na Mbeya kwa kura 59, ambaye baada ya kusikia matokeo alipoteza fahamu kwa furaha.
Nyenzi aliibuka mshindi akiwapiku washindani wake Elias Mwanjala (46), John Kiteve (12) na David Lugenge aliyeambulia kura nane.
Kanda ya Njombe na Ruvuma, ushindi ulikwenda kwa James Mhagama kwa kura 93 akimbwaga Stanley Lugenge aliyepata kura 31 na katika Kanda ya Lindi na Mtwara, Athuman Kambi alishinda kwa kura 84, akiwabwaga Francis Ndulane (30) na Zafarani Damoder 11.
Kanda ya Dodoma na Singida, mshindi ni Hussein Mwamba kwa kura 63, akiwashinda Stewart Masima (58) na Charles Komba aliyeambulia kura nne.
Geofrey Nyange ‘Kabulu’ alishinda kwa Kanda ya Morogoro na Pwani kwa kura 78, akimshinda Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na Twahil Njoki aliyepata kura mbili pekee.
Mshindi kuwakilisha Kanda ya Kilimanjaro, ni Khalid Mohamed kwa kura 69 akimshinda Davis Mosha aliyepata kura 54 huku mshindi wa Kanda ya Dar es Salaam, ni Wilfred Kidau aliyepata kura 60, akimshinda Said Balhabou (50), Omary Isaac (10) na Alex Crispine (4).
Rais Leodegar Chilla Tenga aliyemaliza muda wake baada ya kuliongoza Shirikisho hilo tangu Desemba 27, 2004, alimpongeza Malinzi kwa ushindi na kuahidi kutoa ushirikiano huku akimkabidhi katiba ya Shirikisho hilo na mpira, japo makabidhiano rasmi yatafanyika Jumamosi ya wiki hii.

Sunday, October 20, 2013

Malinzi kuzindua kampeni Jumatano

Malinzi kuzindua kampeni Jumatano
MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema anatarajia kuzindua ilani yake ya Uchaguzi Mkuu Jumatano, kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, huku akiwataka wagombea wa nafasi tofauti kufanya kampeni za kistaarabu.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Malinzi alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa juhudi zao na umakini katika kusimamia mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 27.
“Nichukue fursa hii kuwatakia kila la kheri wagombea wote, niwatakie kampeni njema, kampeni zenye wingi wa baraka na fanaka tele, na nina imani tutafanya kampeni za kistaarabu zisizoonyesha hisia za ubaguzi wa dini, kabila, jinsia au ueneo,” alisisitiza Malinzi.

Azam yashika usukani Ligi Kuu Vodacom

Azam yashika usukani Ligi Kuu Vodacom
AZAM FC imekaa kileleni mwa Ligi Kuu, baada ya jana kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro na kufikisha pointi 20 katika mechi kali iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Bao hilo pekee lilifungwa na Hamis Mcha dakika ya 79, kutokana na mpira wa adhabu iliyokwenda moja kwa moja.
Kutoka Turiani, Morogoro, Mtibwa Sugar imepanda hadi nafasi ya nne ikifikisha pointi 16 baada ya kuichapa Mgambo Shooting mabao 4-1.
Kutoka Uwanja wa Sokoine Mbeya kuwa Mbeya City, nayo imefikisha pointi 20, hivyo kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.
Bao la vijana hao wa Kocha Juma Mwambusi, lilipachikwa wavuni na Jeremiah John katika dakika ya 36, baada ya kufanya shambulizi kali langoni mwa JKT Ruvu.
Katika Uwanja wa Azam Complex, Ashanti United imetoka sare ya 2-2 na Ruvu Shooting.

Monday, October 14, 2013

Mkongwe Van der Sar amfagilia De Gea

Mkongwe Van der Sar amfagilia De Gea
KIPA wa zamani wa Manchester United, Edwin van der Sar amemsifu kipa namba moja wa timu hiyo, David de Gea, akisema ni miongoni mwa nyota ambao wataisaidia timu hiyo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
De Gea ni kipa aliyeonesha uwezo mkubwa langoni tangu kuanza kwa msimu huu ikiwemo katika mechi dhidi ya Sunderland walipotoka nyuma na kushinda 2-1.
Wakicheza nyumbani, Sunderland walitangulia kupata bao dakika ya tano likipachikwa wavuni na Emanuele Giaccherini kabla ya Januzaj kufunga mawili dakika za 55 na 61.
Katika mechi hiyo, mrithi huyo wa Van Der Sar, aliyetua Old Traffod kwa dau kubwa wakati huo akiwa na umri wa miaka 20, alionesha uwezo mkubwa langoni.
"Huwezi kuamini," alisema kipa huyo wa zamani wa Man Utd, ambaye sasa ni Meneja Masoko wa klabu ya Ajax ya Uholanzi na kuongeza kuwa, ameweza kucheza ligi tofauti akiwa na umri mdogo.
"Alitua Old Trafford kutokea Hispania akiwa hawezi kuzungumza kiingereza na kula chakula tofauti, mbinu tofauti na mazoezi tofauti, lakini ameweza kukabiliana nayo.
"Upigaji wa soka ya England katika kona na adhabu ya nje na ndani ya boksi, ni tofauti kabisa na Hispania, kwa vyovyote alipata ugumu kuzoea katika siku za awali,” alisema akimfagilia kipa huyo.
Alisema kwa vile bado ni kijana mdogo, kipa huyo ataopata mafanikio makubwa katika maisha yake ya soka kwani kwa kipindi alichodumu Old Trafford, atakuwa amejifunza mengi."

Sunday, October 13, 2013

Neymar moto wa kuotea mbali Brazil

Neymar moto wa kuotea mbali Brazil
BRAZIL chini ya Kocha wake Luiz Felipe Scolari, jana iliichapa Korea Kusini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, ukiwa ni ushindi wa tatu mfululizo kabla ya kuikabili Zambia, Jumanne ijayo katika mechi nyingine ya kimataifa.
Mabao ya wenyeji hao wa fainali za Kombe la Dunia za mwakani, yalifungwa na Neymar na  Oscar.
Neymar alifunga bao lake mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa mpira wa adhabu ya moja kwa moja na kumtungua kipa Jung Sung-Ryong kabla ya Oscar  kufunga jingine kwa shuti kali.