Tuesday, July 30, 2013

Robben awatuliza wenzake Bayern 
MCHEZAJI mahiri wa Bayern Munich, Arjen Robben, amewaambia wachezaji wanzake hawana sababu ya
‘kupaniki’ kwa kufungwa mabao 4-2 na wapinzani wao, Borussia Dortmund, katika mechi ya Supercup.
Kipigo hicho cha mwishoni mwa wiki kwa kiasi kikubwa kimewachanganya Bayern wakizingatia ni mechi ya ufunguzi wa Bundesliga, tena wakiwa chini ya Kocha mpya, Pep Guardiola.
Zaidi ya hilo, kipigo hicho ni kama kuwadhalilisha wakali hao waliomaliza msimu uliopita wakiwa na mataji matatu,  Bundesliga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ujerumani.
Aidha, kipigo katika mechi hiyo ya kuukaribisha msimu mpya wa Bundesliga, kumemzuia Kocha mpya, Pep Guardiola kuonja radha ya ubingwa kabla ya kuanza kwa Bundesliga.
Katika mechi hiyo, Borussia chini ya Kocha wake, Jurgen Klopp, walionesha soka ya nguvu kiasi cha kuwafunika mabingwa hao wa Ulaya, matokeo ambayo yameonekana kuwavunja moyo baadhi yao.
“Hatuna sababu ya ‘kupaniki’, tuangalie kiwango chetu, kwa upande wangu sina hofu kabisa,” alisema Robben alipozungumza na mtandao wa TZ huku akiwapongeza Borussia kwa kucheza vizuri.
“Nawapongeza Dortmund. Walistahili kushinda. Lakini kufungwa kwetu hakuna maana kuwa tumecheza hovyo.
“Sidhani kama mabao manne yametokana na staili yetu ya kushambulia katika mechi ile, hatupaswi kupoteza muda kufikiria kipigo, tujifunze kutokana na makosa.
Mabingwa Bayern wataanza kampeni ya kutetea taji la Bundesliga Agosti 10 kwa kuwakaribisha Greuther Furth.

No comments:

Post a Comment