Friday, July 26, 2013

Kashfa ya dawa inakera - Usain Bolt
BINGWA mara sita wa Olimpiki, Usain Bolt wa Jamaica, amesema anakabiliwa na jukumu zito la kuurejeshea heshima mchezo huo kitaifa na kimataifa baada ya nyota wenzake kuingia kwenye tuhuma za kutumia dawa za kusisimua misuli miezi miwili iliyopita.
Kauli hiyo imekuja huku wachezaji mahiri wa mbio fupi,
Asafa Powell wa Jamaica na Tyson Gay ambao wameangukia kwenye tuhuma hizo wakiungana na Sherone Simpson ndani ya mwaka huu.
Bolt (26), aliyeshiriki mbio za hisani wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Olympic, alisema ni jukumu lake na wachezaji wengine kufanya kweli ili kufukia kashfa hiyo katika riadha.  
"Nina kazi kubwa ya kufanya kufukia kashfa hii katika nchi yangu," alisema Bolt na kuongeza:
"Kwa sasa nimeelekeza nguvu katika hilo na kuwadhihirishia watu kuwa mafanikio na ushindi vyote vinawezekana katika mchezo huu."
Bolt aliyesisitiza kuwa yeye ni mtu safi kutokana na kutowahi kupatwa na kashfa ya kutumia dawa, lakini akasema yahitaji mtu kuwa mwangalivu sana asiangukie kwenye mkasa huo.
Bolt, bingwa wa mbio fupi katika mita 100 na 200, alisema kufanya kwake vizuri tangu akiwa kijana mdogo, ni uthibitiosho kuwa yeye ni mtu safi asiyetumia dawa za kuongeza nguvu.
"Nimewahi kuvunja rekodi nikiwa kijana mdogo ambayo hadi sasa haijavunjwa," alisema Bolt alipozungumza na BBC.
Nyota huyo alitumia nafasi hiyo kuueleza ulimwengu kuwa, amekuwa akipata mafanikio kutokana na kipaji kutoka kwa Mungu na juhudi katika mazoezi. 

No comments:

Post a Comment