Tuesday, July 30, 2013

Kazimoto afaulu majaribio Qatar
KLABU ya Al Markhiya Sports Club ya Doha, Qatar imetuma barua kwa uongozi wa Simba ukiomba umruhusu kiungo wake Mwinyi Kazimoto kujiunga na timu hiyo baada ya nyota kufanya vizuri katika majaribia yake hivi karibuni.
Habari za uhakika zinasema, Kazimoto aliyekwenda Qatar wiki iliyopita kusaka nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu hiyo, ameshafanyiwa vipimo vyote hivyo kinachotakiwa ni kibali tu kwa ajili ya kuichezea timu hiyo iliyoasisiwa mwaka 1995 ambayo sasa inacheza Ligi Daraja la Pili.
Japo nyota huyo aliondoka bila idhini ya viongozi wa Simba wala wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) kutokana na kuondoka nchini akitokea kambi ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars,  Al Markhiya imeiangukia Simba kuomba ridhaa yake.
Tanzania Daima ilipoutafuta uongozi wa Simba kuhusu jambo hilo, kiongozi mmoja wa Simba alikiri kuwepo kwa barua hiyo iliyoandikwa na Mohamed Abu Ali, lakini wenye mamlaka juu ya uamuzi huo ni viongozi wa juu wa klabu.
“Kweli kuna hiyo kitu, lakini siwezi kulizungumzia kwa undani zaidi kwani sina uamuzi juu ya hili na hasa ikizingatiwa mazingira ambayo mchezaji mwenyewe aliondoka sasa tuwaachie viongozi wenye mamlaka,”alisema
Hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa juu wa  Simba aliyeweza kupatika jana baada ya kutopokea simu zao za viganjani.
Kama Kazimoto atapata baraka kutoka kwa uongozi wa Simba atakuwa ni miongoni mwa nyota wa Tanzania wanaopata ulaji wa kutakata kupitia soka la kulipwa.
Kiiza kubanwa Jangwani
WAKATI nyota wake wa kimataifa, Mganda Hamis Kiiza, alitarajiwa kuwasili jana, uongozi wa Yanga umepanga kumbana awapatie barua ya klabu aliyokwenda kufanya majaribio nchini Serbia kabla ya kumatia mkataba mpya.
Usajili wa Kiiza umegubikwa na utata kutokana na nyota huyo  kuhitaji dau la sh mil. 45 huku uongozi ukitaka kumpa sh mil. 35 kwa mafungu, jambo ambalo linapingwa na nyota huyo.
Habari kutoka katika klabu hiyo zimedokeza kama mchezaji huyo atarejea na barua anaweza kusaini mkataba mpya wa Mil. 35 na kwamba si zaidi ya kiasi hicho.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa Kiiza amekuwa akiwachanganya vichwa kwani amekuwa akihitaji mshahara si chini ya dola 1,000 na dola 2,000 za usajili kwa kila mwezi.
Maradona atoa dozi kwa mpiga picha
Maradona (kulia) akimshambulia kwa mateke mpiga picha
MPIGA picha wa jarida maarufu amefungua jalada kituo cha polisi, akimtuhumu nguli wa zamani wa soka la hapa Diego Maradona kumshambulia kwa mateke kinenani katika tukio tata lililoacha maswali.
Mpiga picha huyo wa kiume aitwaye Enrique Medina, ameripoti kushambuliwa na mkongwe huyo Jumapili usiku akiwa nje ya nyumba ya baba yake Maradona, wakati alipoweka kambi ya muda kusubiri kumpiga picha mshindi huyo wa Kombe la Dunia 1986.
Medina aliliambia Shirika la Habari la Associated Press Jumatatu kuwa Maradona alikimbia kana kwamba ‘anayeenda kupiga mpira wa adhabu ndogo,’ na kisha akampiga yeye teke kali kinenani na juu ya mguu na kumsababishia maumivu makali.
“Halikuwa teke la mtu wa kawaida,” alisema Medina na kuongeza: “Lilikuwa teke kutoka kwa mtu anayejua hasa kupiga mateke ... Alionekana kuwa na hasira hasa, aliyekosa utu kwa muda. Lilikuwa ni tukio lililotokea katika nyumba ya baba yake.”
Mara kadhaa Maradona amevilalamikia vyombo vya habari kuwa vinamfuatilia sana hadi maisha yake ya ndani. Mwaka 1994, aliwahi kuwafyatulia risasi hewani wanahabari na kujikuta akifungiwa miaka miwili wakati huo akiichezea Newlle’s Old Boys.
Mei mwaka huu, Maradona aliwahi kuliacha gari katika barabara kuu na kuokota mawe na kuanza kuwarushia wapiga picha waliokuwa wakimfuatilia kutoka Uwanja wa Ndege kwenda nyumbani kwao.
Tukio la juzi, limetokea wakati Maradona aliporejea Argentina kutoka Dubai anakofanya kazi kama Balozi wa Soka Falme za Kiarabu.
Wadhamini Stars mwendo mdundo
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe akimkabidhi zawadi 
ya DVD Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja hivi karibuni
LICHA ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kukosa tiketi ya fainali za Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN) zitakazochezwa mwakani nchini Afrika Kusini kwa kufungwa na Uganda jumla ya mabao 4-1, wadhamini wa timu hiyo, Kilimanjaro Premium Lager wamesema hilo haliwafanyi wakate tamaa.
Meneja wa bia hiyo George Kavishe alisema juzi kuwa japo matokeo hayo si mazuri, lakini ni vizuri Watanzania wakajua kuwa mafanikio ya soka yanahitaji subira.
“Ni vema tukumbuke kuwa kwenye soka kuna kushinda na kushindwa,” alisema Kavishe na kuongeza:
“Tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa sisi kama wadhamini hatujakata tamaa na bado tuna imani na timu hii na kocha Kim Poulsen, kwa hiyo tunawaomba wasife moyo.”
Alisema wakati wanalipoanza kuidhamini timu hiyo Mei, 2012 kwa kuwekeza zaidi ya sh bilioni mbili kwa mwaka, kwa muda wa miaka mitano, walikuwa na malengo mengi likiwemo kuinua hadhi ya timu hiyo na kuhakikisha wanaingia kambini kwa wakati muafaka.
Kavishe alisema jambo hilo ni muhimu kwa ufanisi wa timu na mengineyo kama kulipwa vizuri na kwa wakati, kula na kulala vizuri pamoja na usafiri wa uhakika.
“Tumejitahidi kufanya mambo haya kwani wachezaji sasa hivi wana DVD zenye maelezo yao, tumewapa suti mpya na za kisasa na pia tumewapa basi jipya la kisasa. Mambo haya yote pamoja na mambo wanayofundishwa na kocha Kim yamesaidia kuleta mabadiliko makubwa,” alisema.
Alisema kuna mafanikio mazuri ya timu ya taifa ambayo Watanzania lazima wayakumbuke kama kuzifunga timu kama Zambia, Cameroon, Morocco na Kenya.
Kavishe alisema walipoanza udhamini, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 145 kwa ubora, lakini iliwahi kufika 109 ingawa sasa inashika nafasi ya 121.
 “Haya ni mafanikio makubwa kwani tumesogea hatua zaidi ya 40,” alisema.
Alisema safari ya mafanikio katika mpira ni ndefu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kuongeza kuwa Kim anafanya kazi nzuri ya kuibua vijana.
“Kocha anahitaji kuungwa mkono na sisi sote kuanzia kwa TFF, sisi wadhamini na Watanzania wote. Tunahitaji kuangalia picha kubwa,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba Watanzania tuwe wazalendo wakati huu, hii ni timu yetu na tunatakiwa kujivunia. Vyombo vya habari pia viwe mstari wa mbele kuonyesha uzalendo.”
Alisema mechi dhidi ya Gambia itakayochezwa mwezi Septemba ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia ni muhimu hata kama Tanzania haisongi mbele kwani itasaidia katika ngazi za Fifa.
Fabregas: Sing’oki Barcelona
BARCELONA waliionya Manchester United chini ya kocha David Moyes kuwa wanapoteza muda katika jaribio la kumng’oa Cesc Fabregas Nou Camp kwenda Old Trafford na sasa imedhihirika hivyo.
Kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania, amewaambia marafiki zake wa karibu kuwa yu tayari kwa vita ya kugombea namba na kujihakikishia nafasi katika kikosi cha Barca.
Manchester United tayari ilikwishatoa ofa mbili na zote zikakataliwa na Barcelona, kabla ya sasa kuratibu ofa ya tatu ya pauni milioni 35 ambayo itakuwa rekodi ya klabu.
Fabregas, 26, bado anaongoza orodha ya wakali wanaowindwa na Moyes kiangazi hiki, lakini chanzo cha ndani klabuni Nou Camp kimethibitisha juzi usiku: “Cesc amesifia mno ofa za Man United na anatambua nini thamani ya ofa zao kwake.
“Lakini ni miaka miwili tu tangu alipoondoka England alikokuwa akiichezea Arsenal na hatarajii kuihama tena Barcelona hususan hivi karibuni.
“Amekuwa katika vita akijaribu kuchuana na Xavi Hernandez na Andres Iniesta, ili kufanikiwa kupangwa upande wa pili baada yao, lakini yeye ameshiriki sehemu ya michezo yao na anahitaji nafasi zaidi ya hiyo,” kilifichua chanzo hicho.
Na kocha mpya Barca, Tata Martino, ambaye amechukua mikoba iliyoachwa wazi na Tito Vilanova aliyebwaga manyanga ili kujiuguza kansa ya tezi, amesisitiza kuwa atomruhusu kijana wake huyo kwenda popote.
Martino alisema: “Man United wanamtaka Cesc? Kama wamekataliwa ofa zao mbili za kumpata, watambue kuwa nitakataa na ofa yao ya tatu pia. Cesc atakuwa nasi hapa,” alisisitiza Martino raia wa Argentina.
Fabregas juzi aliripotiwa kuungana na wenzake katika kambi ya kujiandaa na msimu mpya na alifanyiwa vipimo vya afya kabla ya msimu kisha kujumuika na wenzake.
Klabu Ligi Kuu Bara zaishangaa Yanga
Kikosi cha Yanga SC
SIKU moja baada ya uongozi wa Yanga kugomea haki za Ligi Kuu ya Bara kuhodhiwa na Azam TV, uongozi wa Azam Media wanaomiliki wa televisheni hiyo, umesema kujitoa kwao hakuna athari katika mchakato wa suala hilo ambalo limepokewa kwa furaha na klabu nyinmgine za ligi hiyo.
Kauli hiyo imetolewa jana na kiongozi wa Azam TV, Said Mohamed ikiwa ni siku moja tangu uongozi wa Yanga kugomea suala la haki za ligi hiyo kumilikiwa na Azam TV kwa hoja kuwa mchakato huo haukuwa wazi na suala hilo lingefanyika baada ya uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania.
Yanga walikwenda mbali zaidi wakisema wao hawastahili kupata mgao sawa na timu nyingine katika mkataba huo kutokana na kuchangia mapato makubwa tofauti na nyingine katika ligi hiyo, hivyo wanastahili kupata mgawo mkubwa zaidi na kuongeza kurusha mechi kutapunguza mapato.
Chini ya mkataba huo wenye thamani ya sh bil 5.6 kwa kipindi cha miaka mitatu, kila klabu itapata kiasi cha sh mil 25 kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Agosti 24 na baada ya kwisha kwa ligi hiyo, kila moja itapata sh mil 75.
Akizungumzia tamkoa la Yanga, Mohamed alisema kujitoa kwa Yanga katika suala hilo, hakutaaathiri mchakato wake wakiamini udhamini huo ni wenye tija kwa klabu za Ligi Kuu ambazo zimekuwa zikilemewa na gharama kubwa za uendeshaji.
Alisema kama Yanga watajitoa, hawataathiri uwepo wa udhami huo kwani watakachofanya ni kurusha mechi 13 za ugenini za timu hiyo na kuachana na mechi za nyumbani ambazo watakuwa na haki nazo kisheria.
“Kama kweli Yanga wataamua kujitoa, haina shida…. hatuwezi kuwalazimisha. Tutakachofanya ni kutorusha mechi ambazo wao watakuwa nyumbani, lakini zile za ugenini zitarushwa kama kawaida kwa mfano Shooting vs Yanga,” alisema Mohamed na kusema anaamini mpango huo ni ukombozi kwa kwa timu nyingine za ligi hiyo na kuongeza:
“Ligi Kuu ina timu 14….kama Yanga wataamua kujiweka kando na mkataba huo, bado hakutaathiri kitu maadamu klabu nyingine ni ukombozi mkubwa kwao, hivyo tutakuwa hatuzitendei haki nyingine ambazo kwa miaka mingi timu zimekuwa zikilemewa na mzigo
wa uendeshaji,” alisisitiza.
Wakati Yanga wakipinga udhamini huo, uchunguzi wa Gazeti hili umebaini kuwa klabu nyingi za Ligi Kuu zimeupokea kwa mikono
miwili kwa hoja kuwa walau sasa zitapunguza matatizo kwa kwani kiasi cha sh mil 100, nje ya nauli na vifaa kutoka kwa mdhamini
mkuu wa ligi hiyo, kampuni ya Vodacom, kutazipunguzia klabu makali ya ukata.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa klabu za Coastal Union, Ashant United na Ruvushooting, wametamka wazi kuwa mkataba huo ni ukombozi mkubwa sio kwao tu, bali kwa klabu zote za Ligi Kuu na soka
ya Tanzania na kwenda mbali zaidi wakisema Yanga wana agenda yao binafsi.
Katibu Mkuu wa Ashant United iliyopanda daraja msimu huu, Abubakar Silas alisema kiasi cha sh mil 100 kwa kila klabu kwa msimu, ni ukombozi mkubwa kwa klabu kwani zitawasaidia kufanya mambo yao bila ya ubabaishaji, hivyo kuongeza hata ushindani wa soka uwanjani kutokana na ukweli kuwa ukata kuchangia timu kufanya vibaya.
“Ukweli ni kuwa, Azam TV ni mkombozi wa soka la Tanzania. Naamini kwa udhamini huu, kwetu Ashant Utd tutafanya mambo makubwa katika ligi kwani haijawahi kutokea kila timu ikapata kiasi hicho cha fedha, umefika wakati sasa watu wakubali mabadiliko kama kweli tunataka kupiga hatua,” alisema Silas.
Naye Ofisa habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema hofu kubwa ya Yanga, ni kuhofia changamoto kisoka kwani kila timu sasa itakuwa fti kifedha tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyopita ambapo kwa kiasi kikubwa timu kubwa zilikuwa na ufanuu mkubwa kupitia mapato ya milangoni na udhamini binafsi.
“Kitendo cha Azam TV kudhamini Ligi Kuuu ni jambo la kupongezwa badala ya kukatishwa tamaa, hawa Yanga wanaonekana wana agenda yao ambayo haina nia njema na maendeleo ya soka ya Tanzania, kwani hoja zao hazina mashiko.
Naye Ofisa Habari wa Coastal Union, Edo Kumwembe alisema wamepokea udhamini huo wa kihistoria ambao haujawahi kutokea katika soka ya Tanzania na kuongeza kuwa kama watu wataweka kando unafiki na kuzungumza ukweli, hata kama ungekuwa wa thamani ya sh mil 50, bado ni wenye tija kwa klabu nyingi katika ligi hiyo.
“Tena huu ni mwanzo…hapo baadae tunaweza kukaa kuuboresha zaidi, jamani kuna timu ambazo zimekuwa zikisajili kwa shida, achilia mbali sisi wenye udhamini wa Binslum, kuna timu zina ukata mkubwa, inaonekana wazi Yanga hawa wana jambo,” alisema Kumbwembe.
Naye Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema hawawezi kutoa kauli yoyote juu ya uamuzi wa Yanga kwani bado halijafikishwa kwao kimaandishi, lakini alionesha kushngazwa na kali kuwa Yanga haikushirishwa kwenye mchakato wa jambo hilo.
“Hatujapokea barua ya Yanga, tutakuwa katika nafasi nzuri ya kulizungumzia hilo baada ya kuona msingi wa madai. Lakini kwa hoja kuwa hawakuwa na mwakilishi, si kweli Katibu Mkuu Mwalusako (Laurance) na Makamu Mwenyekiti  Sanga (Clement) wameshiriki kubariki maamuzi ,” alisema Wambura.
Kuhusu hoja kwanini jambo hilo lisifanyike baada ya uchaguzi mkuu, Wambura alisema TFF iliamua kugawa majukumu yaliyowapa nguvu Kamati ya Ligi kukaa mezani kujadili udhamini huo chini ya dhama ya mgawanyo wa majukumu ambapo si Shirikisho hilo kufanya kila kitu.
Messi atwaa tuzo Ulaya
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina anayecheza katika klabu ya FC Barcelona ya hapa, Lionel Messi, amefurahia kutwaa tuzo ya nyota aliyefunga zaidi ya mabao 50 kwa msimu uliopita.
Messi ambaye pia anashikilia rekodi ya kuwa nyota bora wa dunia
mara nne mfululizo, ametwaa tuzo hiyo kwa mara ya tatu akiwabwaga mkongwe Gerd Muller aliyewahi kufunga mabao 85, rekodi ambayo  ilidumu kwa miaka 40
Katika msimu uliopita, Messi (26), aliivunja rekodi hiyo kwa kufunga mabao 91 kati ya 313 yaliyofungwa na timu yake kwa msimu.
Kwa upande wa Messi, si mara ya kwanza kutwaa tuzo hiyo kwani alifanya hivyo pia katika miaka ya 2009 na 2011.
Nyota wengine waliowahi kutwaa tuzo hiyo kwa kufunga mabao mengi kwa msimu, ni Cristiano Ronaldo (2008), Wesley Sneijder (2010), na Cristiano 2012.
Mbali ya kufunga mabao mengi, Machi mwaka huu Messi aliweka rekodi ya kufunga mabao katika mechi 19 mfululizo La Liga, ikiwa ni rekodi ya ya aina yake katika ligi kuu.
Baada ya kutwaa tuzo hiyo, Messi alisema: “Nimefurahi sana kwa mafanikio haya. Kama wachezaji,  tulifanya kazi kubwa kuipatia heshima timu, tuzo hii haikustahili kuja kwangu, bali kwa timu nzima.”
Tuzo hiyo ambayo imekuwa ikiratibiwa na mtandao wa Goal, mshindi amekuwa akipigiwa kura na waandishi wa habari wapatao 500 kwa kushindanisha nyota bora 50.
Swaumu yatishia mechi ya Al Ahly, Orlando

Kikosi cha Orlando Pirates
MABINGWA wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Ahly ya Misri wametaka mechi yao ya hatua ya makundi ya michuani hiyo dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini iliyokuwa ipigwe Agosti 4, isogezwe mbele kwa siku tano.
Sababu ya Ahly kuomba hivyo, ni kutoa nafasi kwa wachezaji wa timu hiyo wamalize kwanza funga ya mwezi wa Ramadhani.
“Tumeandika barua kuomba iwe hivyo, lakini tunasubiri jibu kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwamba badala ya kuchezwa Agosti 4, ichezwe Agosti 9,” alisema Mkurugenzi wa Ahly, Sayed Abdel Hafiz.
Alisema wamelazimika kuomba hivyo baada ya wachezaji kugoma kufungulia siku hiyo ya mechi, hivyo hawana la kufanya zaidi ya kuomba ridhaa ya Caf.
“Wachezaji wetu wamekataa kutofunga siku ya mechi hiyo kama ilivyokuwa Jumatano iliyopita tulipocheza na Zamalek,” alisema kiongozi huyo ambaye ameonekana wazi kutoridhishwa na matokeo ya sare.
Pamoja na wachezaji kuruhusiwa kutofunga siku za mechi, jambo hilo limekuwa gumu kutekelezwa na wengi, hivyo kuathiri ufanisi wa timu dimbani.
Aidha, Ahly wamelazimika kusaka uwanja mwingine kwa ajili ya mechi hiyo ya kundi A, baada ya Jeshi la Ulinzi linalomiliki uwanja huo kuuzuia kwa mechi hiyo.
Wiki iliyopita, Ahly walianza kampeni ya hatua ya makundi dhidi ya jirani zao Zamalek katika mechi iliyochezwa mjini El-Gouna, kilometa 450 kutoka Cairo kutokana na sababu za kiusalama.
Kikosi cha Al-Ahly
Licha ya vyombo vya usalama kuruhusu mashabiki 7,000 katika uwanja huo wenye uwezo wa watu 12,000, iliisha kwa amani.
Mamlaka za Cairo wana mpango wa kuipeleka mechi hiyo katika mji wa Aswan, uliopo kilometa 870 kutoka Cairo.
Wakati Zamalek na Ahly zikianza kampeni hiyo kwa sare ya bao 1-1, Pirates walitoka sare ya bila kufungana dhidi ya AC Leopards katika mechi za kwanza katika kundi A.
Timu mbili za juu katika hatua ya makundi, zitaingia katika hatua ya nusu fainali kuwania tiketi ya fainali ambapo bingwa atapata tiketi ya kucheza Klabu Bingwa ya Dunia itakayochezwa Desemba mwaka huu nchini Morocco.
Robben awatuliza wenzake Bayern 
MCHEZAJI mahiri wa Bayern Munich, Arjen Robben, amewaambia wachezaji wanzake hawana sababu ya
‘kupaniki’ kwa kufungwa mabao 4-2 na wapinzani wao, Borussia Dortmund, katika mechi ya Supercup.
Kipigo hicho cha mwishoni mwa wiki kwa kiasi kikubwa kimewachanganya Bayern wakizingatia ni mechi ya ufunguzi wa Bundesliga, tena wakiwa chini ya Kocha mpya, Pep Guardiola.
Zaidi ya hilo, kipigo hicho ni kama kuwadhalilisha wakali hao waliomaliza msimu uliopita wakiwa na mataji matatu,  Bundesliga, Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ujerumani.
Aidha, kipigo katika mechi hiyo ya kuukaribisha msimu mpya wa Bundesliga, kumemzuia Kocha mpya, Pep Guardiola kuonja radha ya ubingwa kabla ya kuanza kwa Bundesliga.
Katika mechi hiyo, Borussia chini ya Kocha wake, Jurgen Klopp, walionesha soka ya nguvu kiasi cha kuwafunika mabingwa hao wa Ulaya, matokeo ambayo yameonekana kuwavunja moyo baadhi yao.
“Hatuna sababu ya ‘kupaniki’, tuangalie kiwango chetu, kwa upande wangu sina hofu kabisa,” alisema Robben alipozungumza na mtandao wa TZ huku akiwapongeza Borussia kwa kucheza vizuri.
“Nawapongeza Dortmund. Walistahili kushinda. Lakini kufungwa kwetu hakuna maana kuwa tumecheza hovyo.
“Sidhani kama mabao manne yametokana na staili yetu ya kushambulia katika mechi ile, hatupaswi kupoteza muda kufikiria kipigo, tujifunze kutokana na makosa.
Mabingwa Bayern wataanza kampeni ya kutetea taji la Bundesliga Agosti 10 kwa kuwakaribisha Greuther Furth.
Kim kugeukia chipukizi
Kim Poulsen akiteta jambo na Kepteni wa Stars, Juma Kaseja
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kipigo kutoka kwa Uganda, kimechangiwa na kutokuwepo kwa
baadhi ya nyota.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo irejee juzi usiku ikitokea Uganda ilikofungwa jumla ya mabao 4-1, hivyo kukosa tiketi ya kwenda Afrika Kusini, Kim alisema sababu nyingine hasa mechi ya marudiano ni wengi kuwa katika saumu.
Katika mechi hiyo ya marudiano ambayo ilichezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Namboole, Stars ilifungwa 3-1, ikitoka kuchapwa
bao 1-0, wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kim alisema pengo la Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Shomari Kapombe na Mwinyi Kazimoto, kuliigharimu timu katika mechi hizo mbili zilizotumika kuamua
timu ya kucheza fainali hizo za nyota wa Ligi za Ndani-CHAN.
Kuhusu saumu, alisema wakati mchezaji hutakiwa acheze akiwa ameshiba na kupata
maji ya kutosha, kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa kwenye mfungo, walishindwa kuhimili kishindo kutoka kwa wapinzani wao.
Alisema amesikitishwa na matokeo hayo, lakini amewasihi watanzania wasikatishwe tamaaa badala yake wazidi kuisapoti wakati jitihada zinafanyika za kujenga kikosi cha timu hiyo kuelekea kampeni ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2015.
Kim alisema kipindi hiki atakitumia kuandaa kikosi chake kuelekeza kampeni nyingine za kimataifa akijikita zaidi kwa vijana kupata kikosi bora cha siku zijazo kitakachoweza kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Wakati Kim akisma hayo, wadhamini wa timu hiyo,  Kilimanjaro Premium Lager wamesema hawajakatishwa tamaa na timu hiyo kukosa tiketi zote mbili za Brazil ambako kutachezwa Kombe la Dunia  hapo mwakani na Afrika Kusini kutakakochezwa fainali za CHAN, badala yake wataendele kusapoti harakati za kukuza mchezo huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya Stars kuwasili, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema licha ya habari hizi kutokuwa njema kwa watanzania, ni vizuri kukubali matokeo na kuangalia picha kubwa na malengo ya muda mrefu.
“Ni vyema tukumbuke kuwa kwenye mpira kuna kushinda na kushindwa,” alisema Bw Kavishe na kuongeza: “Tunapenda kuwahakikishia watanzania kuwa sisi wadhamini, hatujakata tamaa, bado tuna imani na timu hii na kocha Kim Poulsen, tunawaomba sapoti zaidi,” alisema.