Sunday, October 20, 2013

Malinzi kuzindua kampeni Jumatano

Malinzi kuzindua kampeni Jumatano
MGOMBEA urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema anatarajia kuzindua ilani yake ya Uchaguzi Mkuu Jumatano, kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, huku akiwataka wagombea wa nafasi tofauti kufanya kampeni za kistaarabu.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Malinzi alitumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa juhudi zao na umakini katika kusimamia mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 27.
“Nichukue fursa hii kuwatakia kila la kheri wagombea wote, niwatakie kampeni njema, kampeni zenye wingi wa baraka na fanaka tele, na nina imani tutafanya kampeni za kistaarabu zisizoonyesha hisia za ubaguzi wa dini, kabila, jinsia au ueneo,” alisisitiza Malinzi.

Azam yashika usukani Ligi Kuu Vodacom

Azam yashika usukani Ligi Kuu Vodacom
AZAM FC imekaa kileleni mwa Ligi Kuu, baada ya jana kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro na kufikisha pointi 20 katika mechi kali iliyochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Bao hilo pekee lilifungwa na Hamis Mcha dakika ya 79, kutokana na mpira wa adhabu iliyokwenda moja kwa moja.
Kutoka Turiani, Morogoro, Mtibwa Sugar imepanda hadi nafasi ya nne ikifikisha pointi 16 baada ya kuichapa Mgambo Shooting mabao 4-1.
Kutoka Uwanja wa Sokoine Mbeya kuwa Mbeya City, nayo imefikisha pointi 20, hivyo kukamata nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu ya Pwani.
Bao la vijana hao wa Kocha Juma Mwambusi, lilipachikwa wavuni na Jeremiah John katika dakika ya 36, baada ya kufanya shambulizi kali langoni mwa JKT Ruvu.
Katika Uwanja wa Azam Complex, Ashanti United imetoka sare ya 2-2 na Ruvu Shooting.