Tuesday, July 30, 2013

Kim kugeukia chipukizi
Kim Poulsen akiteta jambo na Kepteni wa Stars, Juma Kaseja
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kipigo kutoka kwa Uganda, kimechangiwa na kutokuwepo kwa
baadhi ya nyota.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu timu hiyo irejee juzi usiku ikitokea Uganda ilikofungwa jumla ya mabao 4-1, hivyo kukosa tiketi ya kwenda Afrika Kusini, Kim alisema sababu nyingine hasa mechi ya marudiano ni wengi kuwa katika saumu.
Katika mechi hiyo ya marudiano ambayo ilichezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Namboole, Stars ilifungwa 3-1, ikitoka kuchapwa
bao 1-0, wiki mbili zilizopita kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kim alisema pengo la Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta, Shomari Kapombe na Mwinyi Kazimoto, kuliigharimu timu katika mechi hizo mbili zilizotumika kuamua
timu ya kucheza fainali hizo za nyota wa Ligi za Ndani-CHAN.
Kuhusu saumu, alisema wakati mchezaji hutakiwa acheze akiwa ameshiba na kupata
maji ya kutosha, kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa kwenye mfungo, walishindwa kuhimili kishindo kutoka kwa wapinzani wao.
Alisema amesikitishwa na matokeo hayo, lakini amewasihi watanzania wasikatishwe tamaaa badala yake wazidi kuisapoti wakati jitihada zinafanyika za kujenga kikosi cha timu hiyo kuelekea kampeni ya kucheza fainali za Afrika mwaka 2015.
Kim alisema kipindi hiki atakitumia kuandaa kikosi chake kuelekeza kampeni nyingine za kimataifa akijikita zaidi kwa vijana kupata kikosi bora cha siku zijazo kitakachoweza kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.
Wakati Kim akisma hayo, wadhamini wa timu hiyo,  Kilimanjaro Premium Lager wamesema hawajakatishwa tamaa na timu hiyo kukosa tiketi zote mbili za Brazil ambako kutachezwa Kombe la Dunia  hapo mwakani na Afrika Kusini kutakakochezwa fainali za CHAN, badala yake wataendele kusapoti harakati za kukuza mchezo huo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya Stars kuwasili, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema licha ya habari hizi kutokuwa njema kwa watanzania, ni vizuri kukubali matokeo na kuangalia picha kubwa na malengo ya muda mrefu.
“Ni vyema tukumbuke kuwa kwenye mpira kuna kushinda na kushindwa,” alisema Bw Kavishe na kuongeza: “Tunapenda kuwahakikishia watanzania kuwa sisi wadhamini, hatujakata tamaa, bado tuna imani na timu hii na kocha Kim Poulsen, tunawaomba sapoti zaidi,” alisema.

No comments:

Post a Comment