Monday, July 29, 2013

Man Utd kula matapishi ya Pogba
TOVUTI moja ya Kihispania imetoa taarifa ya mshangao kuwa aliyekuwa kiungo wa Man United Paulo Pogba kwamba anaweza akarejeshwa Old Trafford.
Mfaransa huyo alijiunga na Juventus msimu wa mwaka jana majira ya joto.
Hata hivyo, Juve wanaripoti wazi kwamba Juve hawana nia ya kusikiliza ofa inayotolewa kwa ajili ya kiungo huyo.
Pogba aliondoka United kwa sababu ya kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Hivyo wataelekeza nia yao ya kumsajili Pogba endapo watakosa huduma ya Fabregas ambaye Kocha wa Man Utd amesema hawatoongeza tena ofa kwa kiungo huyo wa Barcelona.
Newcastle yanawa mikono kwa Gomis
Bafetimbi Gomis
TIMU ya soka inayoshiriki Ligi Kuu England imejitoa katika mbio zake za kumsajili mshambuliaji raia wa Ufaransa anayeichezea klabu ya Lyon, Bafetimbi Gomis.
Loic Remy
Imefahamika Newcastle waliongeza ofa yao kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 ya paundi milioni 6.9
Hata hivyo upande wa Klabu yake ya Lyon waliikata ofa hiyo wakitaka waongezwe.
Kocha wa Newcastle, Alan Pardew amekuwa na hamu ya kuongezea makali katika safu yake ya ushambuliaji kwa kumsajili Gomis ambaye alifunga mabao 18 katika msimu ulioisha kwa Lyon.
Kwa sasa ameelekeza nguvu yake yakutamani kumsajili mshambuliaji wa QPR Loic Remy kwa mkopo wa  muda mrefu.
Japokuwa anasafu kali ya ushambuliaji inayoongozwa na Waafrika, Shola Ameobi na Papiss Cisse lakini Pardew na uongozi wa klabu yake wanafanya kazi ya kuhakikisha wanaleta sura mpya kwenye klabu hiyo
Yanga yatoa walaka kwa Azam Tv
Rais wa Yanga akizungumza na waandishi wa habari (hawamo pichani)
YAH: URUSHWAJI KATIKA TELEVISHENI MICHEZO YA YANGA.

Hivi karibuni, Tanzania Football Federation (TFF)  iliunda Tanzania Premier League chini ya Bodi yampito Bodi ya TPL ambayo ni msimamizi mpaka hapo Bodi itakayokuwa imechaguliwa kidemokrasia. Bodi hii imeamua peke yake kuingia katika mkataba wa miaka 3 (mitatu) na kampuni inayoitwa Azam Television (ambayo ina  mapromota wale wale wanaomiliki Azam Football Club). Makubaliano ambayo Bodi ya TPL inatarajia kuingia na Azam Television, Kamati ya Utendaji ya YANGA inalipinga kwa nguvu zote katika misingi ifuatayo:

1.         BODI YA TPL

1.1       Bodi iliyoko sasa hivi ni ya mpito ambayo ilitakiwa kutenguliwa na Bodi iliyochaguliwa kidemokrasia kwa kupitia uchaguzi wa tarehe  ……….. mwaka huu na haitakiwi kuingia katika mikataba a miaka mingi wakati inakaribia kuondoka katika ofisi.

1.2       Bodi ya TPL iliyoko sasa hivi haikuchaguliwa kidemokrasia.

1.3       Bodi ya TPL iliyoko sasa hivi haina mjumbe hata mmoja aliyeteuliwa kutoka YANGA.

2.         UTARATIBU WA DUNIA NZIMA

2.1       Haijawahi kutokea katika ligi ya mpira wa miguu ya kisasa kulazimishwa kwa Klabu inayoshindana katika ligi kuachia haki zake za urushwaji wa michezo zichukuliwe na chombo cha habari cha Klabu ya upinzani.

2.2       Mfumo (undertaking) ambao TPL inataka kuanzisha kwa njia ya kulazimisha mkataba kwa YANGA iachie  urushwaji wa michezo yake ya soka yarushwe na Azam TV unatishia sana uwepo wa msingi wa ushindani katika soka ya Tanzania.

2.3       Makubaliano kati ya TPL na Azam Television kuhusu utaratibu wa malipo yanasema kwamba Klabu ya YANGA na Klabu zingine zitakazoshiriki katika Ligi Kuu ya Tanzania  watapata mgao sawa wa mapato ya urushwaji wa michezo hii, ambayo YANGA inapinga kwa sababu kama inavyofanyika duniani kote kwenye ligi zilizofanikiwa (angalau) kutofautisha mgawanyo wa mapato kati ya timu kufuatana na matokeo ya mwisho wa ligi.

2.4       Kamati ya Utendaji ya YANGA siyo tu haikubaliani na mgawanyo sawa wa mapato ambao hautofautishi kati ya timu ya kwanza katika ligi na timu ya mwisho katika ligi, lakini pia ukosefu wa viwango (premiums) vitakavyolipwa:

2.4.1    Vilabu vya mpira vyenye ufuasi wa washabiki wengi;

2.4.2    Vilabu vya mpira vinavyoendeshwa na Wanachama;

2.4.3    Vilabu vya mpira visivyopata ruzuku kutoka Serikalini n.k.

3.         MIGOGORO YA MASLAHI

3.1       Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mpito ya TPL ni Mkurugenzi mwandamizi wa Makampuni ya Azam na  kwa hivyo mazungumzo ya siri kati ya Bodi ya TPL na Azam ni ya kutiliwa mashaka.

3.2       Makampuni ya Azam yana yanashindana kibiashara na makapuni mengi yakiwemo ya utengenezaji wa vinywaji baridi na imeonyesha huko awali inaweka “matakwa maalum” muhimu zaidi kuliko mprira  wa miguu, kama vile Azam F.C. hawashiriki katika Kombe la Tusker na kwa hiyo YANGA inakuwa na msimamo kwamba kwa Azam Television kupewa leseni ya kurusha matangazo ya mpira wa miguu inatishia biashara za washiriki wa sasa na wa baadaye wa YANGA.

3.3       Azam na YANGA wana uadui wa kimichezo. Kumbuka, wakati MRISHO NGASSA alipotaka kwenda YANGA, Azam F.C. walimkopesha kwa nguvu kwa Klabu ya Simba! Kwa hiyo YANGA itahatarika kwa matangazo yenye upendeleo kama Azam Television itarusha hewani michezo yake n.k.

4.         KUTOKUWA NA UWAZI

4.1       Mkataba wa utangazaji wa miaka mingi unaotaka kuingiwa kati ya TPL na ambao bado haujarushwa Television ya Azam haukushindanishwa na vyombo vingi vya habari,  na vyombo ambayo wako tayari kwenye soka havikujulishwa kuhusu fursa hii au walizuiliwa kufikisha mapendekezo yao ya maombi ya haki za kurusha matangazo katika Ligi Kuu (Tanzania Premier League).

4.2       Ukosefu wa uwazi wa TPL unanonyesha kuwa MoU iliyokusudiwa kuwekewa saini na TPL haikufikishwa YANGA kwa ajili ya mapitio ya kisheria, licha ya YANGA kufanya ombi hilo kwaTPL.

5.         MAZINGATIO YA KIBIASHARA

5.1       Mamlaka ya kuamua mzozo wowote wa mkataba wa leseni ya utangazaji wa Ligi Kuu (Tanzania Premier Leagu) itakuwa ni Mahakama ya kisheria na siyo FIFA. TPL inasingizia  kwamba leseni ya matangazo ambayo inakusudia kufanya kuwa ni maagizo ya FIFA na kwa hiyo YANGA inapaswa kuukubali "lock, stock and barrel."

5.2       TPL inaelezea kimakosa makubaliano ya leseni ya urushaji  wa mchezo ya mpira inayotarajia kuingia na Television ya Azam kama "makubaliano ya udhamini" (“sponsorship agreement”) ambayo siyo sahihi, kwa sababu urushaji wa michezo ya mpira wa miguu ni biashara inayotokana na maslahi ya uhusiano na hivyo
wahusika wote ni lazima wazingatie maslahi yao ya kifedha.

Kwa mfano, moja ya vyanzo muhimu vya mapato ya YANGA ni mapato ya kiingilio ya mlangoni yatokanayo na michezo ya mpira wa miguu ambayo urushwaji wa michezo hii itapunguza mapato haya. Kwa wastani michezo ya YANGA  Dar es Salaam huingiza makusanyo ya mlangoni shilingi milioni 50 kwa kila mchezo na hata kushuka kidogo kwa 25% katika mahudhurio ya mechi za YANGA zinafikia mara mbili ya mapendekezo ya mapato takribani Sh milioni 8.3 kwa mwezi kupokelewa na YANGA kutoka mradi wa kibiashara kati ya TPL na Azam Television. Kwa kuzingatia haya, kwamba hata siku za nyuma kama kulikutokea fursa ya kurusha mchuano wa mpira unapochezwa, wadau wote (Timu za mpira wa miguu, TFF na Mtangazaji)  walikuwa wanaafikiana kwanza kwa pamoja kuhusu mapato na mgawanyo wake.

Kamati ya Utendaji ya YANGA ina maoni kwamba makubaliano yoyote ya kibiashara yanayoihusu ni lazima iyalinde maslahi kifendha ya Klabu yake ambapo makubaliano ya TPL / Azam Television hayaangalii na kwa hiyo, Kamati ya Utendaji ya YANGA haitaki mchezo wake urushwe hewani na Azam Television.

Msisitizo wa TPL kuwa lazima Azam Television irushe hewani michezo ya YANGA linasikitisha. Kamati ya Utendaji ya YANGA haina tatizo na Vilabu vingine vya mpira wa miguu zikiruhusu michezo yao kurushwa na Azam Television ila haifurahii kuwa TPL inalazimisha YANGA kuonyesha mchezo wake wa Vodacom Premier League katika Azam Television.
......................
(YUSUF MANJI)
MWENYEKITI
YOUNG AFRICANS SPORTS CLUB

29 JULAI, 2013
Mourinho: Wenger ni mchizi wangu
MAKOCHA wa klabu hasimu za Arsenal na Chelsea, Arsene Wenger na Jose Mourinho, kwa sasa ni kama maswahiba wakubwa, ambapo Mourinho amekiri kuwa anamheshimu mno Wenger licha ya klabu zao kuwa pinzani.
Ukaribu wa Wenger na Mourinho, umeonekana kwa wawili hao kuambatana pamoja wakati wa chakula cha usiku nje ya makazi yao, ambapo Special One amesisitiza kuwa heshima yake kwa Wenger inatokana na mafanikio yaliyotukuka akiwa Arsenal.
Mourinho raia wa Ureno, alisema: “Yeye ni mtu mzuri sana. Namheshimu sana yeye na daima natarajia kuonyesha heshima zaidi kwake.
“Nisingependa kuwa na tatizo lolote baina yetu. Wakati unapokuwa huko katika ligi hiyo na wakati kunapokuwa hakuna mechi baina yetu, ni rahisi mno kuwajua watu.
“Na mimi nilikuwa na nafasi bora zaidi ya kukutana na yeye wakati nilipoondoka England, katika UEFA, michuano ya Euro, Kombe la Dunia. Tulikutana katika chakula cha jioni na ilikuwa ni nyakati nzuri. Nilikuwa nafurahia kuzungumzia soka na yeye.”
Mourinho alienda mbali zaidi na kufichua kuwa yeye anaweza kujifunza kutoka kwa Wenger, namna sahihi ya kudumu na klabu moja kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mreno huyo alisema: “Wenger ananifundisha mimi namna gani ya kudumu hapa kwa miaka 17. Hilo lilikuwa moja agenda wakati wa mazungumzo yetu ya mwisho.
“Kupewa na kupata heshima kama anayopata kutoka kwa bodi ya klabu ni jambo muhimu. Sio kutokana na uso wake nzuri, bali ni kutokana na kazi bomba aliyofanya.
“Alikuwa na nafasi nyingi tu za kutimka Gunners, yote ni kutokana na nia nzuri ya klabu kwake, hivyo wakati akikataa ofa za kuhama na kutaka kubaki Emirates ni kwa sababu anapapenda na sababu ikiwa ni matarajio yake ya baadaye,” alimaliza Mourinho.
Madrid yamvalia njuga Bale
Gareth Bale
MIAMBA ya soka la hapa, Real Madrid, juzi usiku ilipiga hatua inayotajwa kuweza kuwa ya mwisho katika jitihada zake za kupata saini ya winga Gareth Bale wa Tottenham kwa ofa inayofikia thamani ya pauni milioni 95 ikihusisha pesa na wachezaji wawili.
Madrid imeripotiwa kuwa iko tayari kutoa kitita cha pauni milioni 51, sambamba na wachezaji wawili, Angel Di Maria anayethaminishwa kwa dau la pauni milioni 25 na Fabio Coentrao pauni milioni 19 – kufanikisha ililoliita ‘dili la karne.’
Tayari Madrid ilishatoa ofa rekodi ya dunia ya pauni milioni 81 kuomba ridhaa ya kumnasa winga huyo wa kimataifa wa Wales, ambalo lilikataliwa na Spurs na kumshangaza hata mchezaji husika.
Lakini, Rais wa Madrid, Florentino Perez, ameenda mbali zaidi katika ofa mpya ya kujaribu kumfanya Bale kuwa nyota mpya wa The Galactico.
Ofa hii mpya ya Madrid, inatabiriwa kumsukuma Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, ambaye amekuwa mbali, asiyetaka kujadili suala hilo, kuridhia uhamisho huo.
Bale juzi alipaza sauti kumwambia Levy kuwa anahitaji ridhaa ya kwenda kujiunga Madrid, huku akimkumbusha mwenyekiti huyo kukumbuka ahadi kuwa angemruhusu kuhama kama klabu hiyo ya White Hart Lane ingekosa tiketi ya mabingwa Ulaya.
Licha ya kumuomba mwenyekiti kubariki uhamisho wake, Bale, 24, amekana mbinu chafu ya kuishinikiza Spurs kumuuza.
Kocha wa Tottenham, Andre Villas-Boas, anatambulika alivyo shabiki wa winga wa kimataifa wa Argentina, Di Maria, 25 ambaye anaambatanishwa katika jaribio la sasa la Madrid.
Na haitarajiwi kama anaweza kukana kuungana na Mreno mwenzake Coentrao, 25, ambaye anaweza kutumika kama beki/winga wa kushoto - mzalishaji wa mashambulizi ya pembeni kutokea nyuma.
Dortmund yamkaribisha rasmi Guardiola
PEP Guardiola juzi usiku alijikuta akiandika historia ya kuchapwa katika mechi ya kwanza ya kimashindano klabuni Allianz Arena, baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Borussia Dortmund na kutwaa ubingwa wa Supercup.
Bayern Munich, ambayo iliichapa Dortmund katika fainali ya Mabingwa Ulaya Mei mwaka huu kwenye dimba la Wembley jijini London, ilishindwa kumzuia Marco Reus kufunga mara mbili na kuipa Dortmund ubingwa ndani ya Uwanja wa Westfalenstadion.
Wakati Bayern ikishindwa kurejea ilichofanya katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mholanzi Arjen Robben – ambaye alifunga bao la ushindi Wembley, alimudu kurejea hilo kwa kufunga mabao yote mawili juzi.
Akizungumzia pambano hilo baada ya filimbi ya mwisho, Guardiola alisema: "Ingawa tumepoteza pambano hili, bado sihisi kuwa Dortmund walikuwa bora kuliko sisi.
"Tuna siku 10 kabla ya ufunguzi wa msimu wa Bundesliga, hivyo tuna muda wa kusahihisha makosa madogo madogo yaliyotugharimu katika mechi hii," aliongeza Guardiola.
Guardiola, ambaye alitwaa jumla ya mataji 13 katika miaka yake minne ya kuinoa FC Barcelona aliyoiacha mwaka jana, ana kibarua kigumu kudumisha makali yaliyoachwa na kocha aliyechukua nafasi yake Jupp Heynckes klabuni hapo.
Chini ya Heynckes, Bayern iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ‘Bundesliga,’ Mabingwa Ulaya na Kombe la Ujeruman (DFP Pokal), iliyotwaa msimu uliopita.
Bayern ambayo ilicheza bila nyota wake Franck Ribery na Bastian Schweinsteiger, huku ikimkosa pia Mario Gotze – aliyetua hapo akitokea Dortmund, hiki ni kipigo chake cha kwanza wakati huu wa maandalizi kuelekea msimu mpya.
Kabla ya hapo, Bayern ilizichapa Fanclub Wildenau mabao 15-1, TSV Regen 9-1, Paulaner Dream Team 13-0, Brescia 3-0, Sonnehof Grossapac 6-0, Hansa Rostock 4-0, Hamburg 4-0, Borussia Monchengladbach 5-1, kabla ya kuichapa Barcelona mabao 2-0.
Kwa upande wake kocha wa Dortmund, Jurgen Klopp alisema: "Ilikuwa ni mechi kubwa, timu zote zikipanda kushambulia na kujilinda vema, kana kwamba hakuna kesho.
“Jambo la msingi ni kuwa Bayern sio wapinzani wetu pekee, tumejibidisha kama sisi.”
Bayern inatarajia kufungua msimu wa Bundesliga kwa kuwavaa Borussia Monchengladbach Ijumaa ya Agosti 9, wakati Dortmund itaumana na Augsburg siku baadaye.
Simba wamvutia kasi Oloya
Moses Oloya
KLABU ya Simba inamsubiri kiungo wa kimataifa wa Uganda, Moses Oloya avunje mkataba na Saigon Xuan Than ya Vetinam ili impatie mkataba wa kuitumikia kwa msimu ujao.
Hiyo inakuja siku chache baada ya kuwatimua nyota wanne wa kigeni kutokana na kutorishishwa na viwango vyao ambao ni Mussa Mudde, Assumani Buyinza, Samuel Ssenkoomi, Felix Cuipo na James Kun.
Kutemwa kwa nyota hao, kunaifanya Simba kusaliwa na wageni wawili ambao ni kipa Abel Dhaira na mshambuliaji mpya Amissi Tambwe, raia wa Burundi anayetarajiwa Siku ya Simba (Simba Day) itakayofanyika mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Pope, wiki iliyopita alizungumza na Oloya na kuahidi atakuja nchini baada ya kuvunja mkataba wake
na Saigon.
“Ijumaa wiki iliyopita, nilizungumza naye (Oloya), akaniambia yuko katika hatua za mwisho kuvunja mkataba wake, baada ya kufanikiwa hilo atakuja kusaini rasmi Simba,” alisema na kuongeza kuwa msimu huu wameamua kufanya usajili kwa utulivu mkubwa.
Pope alisema kama watafanikiwa kupata saini kiungo huyo, wanaimani msimu ujao watakuwa na kikosi imara hivyo kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu kutokana na uwezo wa mchezaji huyo.
Alisema hata kama itatokea wakamkosa nyota huyo kwa ajili ya raundi ya kwanza ya ligi hiyo itakayoanza Agosti 24, watahakikisha wanafanikisha wanakuwa naye katika raundi ya pili kutokana na mchezaji huyo kukubali kutua Msimbazi.
Oloya, kiungo alitezaliwa Oktoba 22, mwaka 1992, kabla ya kutimkia Vietnam, msimu wa 2009/10 aliichezea KCC ya Uganda kabla ya kutua Saigon mwaka 2011 na kuichezea mechi 29 hadi sasa, akifunga mabao matano. Ameichezea Uganda mechi 22.
Kipigo cha Stars chagusa wadau
Wachezaji wa Uganda wakishangili moja ya bao walipokutana na Stars
SIKU moja baada ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kuikosa tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa nyota wa ligi za ndani (CHAN) kwa kufungwa na Uganda mabao 4-1, wadau wamekuwa na maoni tofauti juu ya sababu ya kufungwa na nini kifanyike.
Kwa kipigo hicho, Stars chini ya kocha wake Kim Polsen imeshindwa kwenda nchini Afrika Kusini ambako kutachezwa fainali hizo mapema mwakani, ikiwe ni pigo jingine kwa tiumu hiyo baada ya kukosa tiketi ya Kombe la Dunia, pia mwakani nchini Brazil.
Ally Hassan Msumari ametoa lawama kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) akisema limekuwa sehemu ya kushindwa huko kwa kushindwa kuiandaa vizuri timu hiyo ambayo wadau waliipa nafasi ya kwenda Afrika Kusini.
Alisema tatizo jingine la timu hiyo ni benchi la ufundi kuwakumbatia baadhi ya wachezaji licha ya kutokuwa na uwezo mkubwa kutokana na kuchoka na kupendekeza mabadiliko katika benchi la ufundi.
Naye Magige Flaviani alihoji uwezo wa Kim akisema ni wakati wa kuachia ngazi kuwapisha wengine wenye uwezo wa kuipatia timu hiyo mafanikio zaidi kwani tayari ilishaanza kupendwa na wengi.
Ally Hoza kwa upande wake alisema sababu ya kufungwa kwa Stars katika mechi zote mbili dhidi ya Uganda, ni wachezaji kuzidiwa kutokana na aina ya maandalizi waliyopewa.
Maoni hayo ya wadau yamekuja huku wachezaji wa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Larger, wakipewa matunzo bora zaidi ikilinganisha na ilivyokuwa zamani.
Msafara wa timu hiyo ulitarajiwa kurejea nchini jana usiku majira ya saa 4 huku kocha wake (Kim) akisema wamekubali matokeo na kilichobaki ni kujipanga kwa kampeni zijazo.