Wednesday, October 2, 2013

Rufani Kamati ya Maadili hitimisho ni leo

Rufani Kamati ya Maadili hitimisho ni leo
SIKU tatu za walalamikiwa waliofikishwa kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukata rufaa zinafikia tamati leo, baada ya wahusika saba kupewa taarifa ya maandishi juzi.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Maadili, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura (pichani), alisema walalamikiwa wote ambao masuala yao ya kimaadili yalifikishwa kwa kamati hiyo, wamearifiwa kimaandishi na wanajua leo ndio mwisho wa kukata rufaa kama hawajaridhika.
Wambura, aliwataja walalamikiwa hao kuwa ni Kamwanga Tambwe, Nazarius Kilungeja, Omar Abdulkadir, Richard Rukambura, Riziki Majala, Shaffih Dauda na Wilfred Kidau.
Kwa mujibu wa kanuni za maadili, wale ambao hawakuridhika na uamuzi huo wa Kamati ya Maadili wanatakiwa kukata rufaa Kamati ya Rufani ya Maadili ya TFF, inayoongozwa na Jaji Mstaafu Stephen Ihema ndani ya siku tatu zinazomalizika leo.
Wambura aliongeza kuwa rufani kwa watakaoamua kufanya hivyo zinatakiwa ziwasilishwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kabla ya saa 10 alasiri ya leo na baada ya hapo hazitapokelewa.
Kwa mujibu wa kanuni ya 74 (1) na (2) ya kanuni za maadili, rufani zote zikionyesha sababu za kupinga uamuzi wa kamati husika, zinatakiwa kuwasilishwa ndani ya siku tatu kwa njia ya posta kwa sekretarieti.
Aliongeza kuwa rufani hizo zinatakiwa kila moja kuambatanishwa na risiti ya malipo ya ada ya rufani, ambayo ni sh milioni moja.
Aidha Wambura aliongeza kuwa Kamati ya Uchaguzi imelazimika kufanya mabadiliko madogo katika ratiba zake za uchaguzi wa Bodi ya Ligi na ule wa TFF chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwezi huu.
Wambura alibainisha kuwa mabadiliko hayo yametokana na ombi la Kamati ya Maadili, iliyotumia muda mrefu kutolea uamuzi hukumu za kimaadili zilizofika mezani kwao, ingawa uchaguzi wa TPL bado utafanyika Oktoba 18, kisha wa TFF Oktoba 27.

No comments:

Post a Comment