Tuesday, July 30, 2013

Wadhamini Stars mwendo mdundo
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe akimkabidhi zawadi 
ya DVD Nahodha wa Taifa Stars Juma Kaseja hivi karibuni
LICHA ya timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kukosa tiketi ya fainali za Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN) zitakazochezwa mwakani nchini Afrika Kusini kwa kufungwa na Uganda jumla ya mabao 4-1, wadhamini wa timu hiyo, Kilimanjaro Premium Lager wamesema hilo haliwafanyi wakate tamaa.
Meneja wa bia hiyo George Kavishe alisema juzi kuwa japo matokeo hayo si mazuri, lakini ni vizuri Watanzania wakajua kuwa mafanikio ya soka yanahitaji subira.
“Ni vema tukumbuke kuwa kwenye soka kuna kushinda na kushindwa,” alisema Kavishe na kuongeza:
“Tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa sisi kama wadhamini hatujakata tamaa na bado tuna imani na timu hii na kocha Kim Poulsen, kwa hiyo tunawaomba wasife moyo.”
Alisema wakati wanalipoanza kuidhamini timu hiyo Mei, 2012 kwa kuwekeza zaidi ya sh bilioni mbili kwa mwaka, kwa muda wa miaka mitano, walikuwa na malengo mengi likiwemo kuinua hadhi ya timu hiyo na kuhakikisha wanaingia kambini kwa wakati muafaka.
Kavishe alisema jambo hilo ni muhimu kwa ufanisi wa timu na mengineyo kama kulipwa vizuri na kwa wakati, kula na kulala vizuri pamoja na usafiri wa uhakika.
“Tumejitahidi kufanya mambo haya kwani wachezaji sasa hivi wana DVD zenye maelezo yao, tumewapa suti mpya na za kisasa na pia tumewapa basi jipya la kisasa. Mambo haya yote pamoja na mambo wanayofundishwa na kocha Kim yamesaidia kuleta mabadiliko makubwa,” alisema.
Alisema kuna mafanikio mazuri ya timu ya taifa ambayo Watanzania lazima wayakumbuke kama kuzifunga timu kama Zambia, Cameroon, Morocco na Kenya.
Kavishe alisema walipoanza udhamini, Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 145 kwa ubora, lakini iliwahi kufika 109 ingawa sasa inashika nafasi ya 121.
 “Haya ni mafanikio makubwa kwani tumesogea hatua zaidi ya 40,” alisema.
Alisema safari ya mafanikio katika mpira ni ndefu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu na kuongeza kuwa Kim anafanya kazi nzuri ya kuibua vijana.
“Kocha anahitaji kuungwa mkono na sisi sote kuanzia kwa TFF, sisi wadhamini na Watanzania wote. Tunahitaji kuangalia picha kubwa,” alisema na kuongeza:
“Nawaomba Watanzania tuwe wazalendo wakati huu, hii ni timu yetu na tunatakiwa kujivunia. Vyombo vya habari pia viwe mstari wa mbele kuonyesha uzalendo.”
Alisema mechi dhidi ya Gambia itakayochezwa mwezi Septemba ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia ni muhimu hata kama Tanzania haisongi mbele kwani itasaidia katika ngazi za Fifa.

No comments:

Post a Comment