Saturday, July 20, 2013

Luis Suarez
Madrid yaiharibia Arsenal kwa Suarez
WAKATI mshambuliaji Luis Suarez akiwakabili Liverpool kufanya nao mazungumzo ya ana kwa ana kuomba ridhaa ya kuhama, imeelezwa kuwa Arsenal wanakabiliwa na vita ya pili na Real Madrid, baada ya miamba hiyo kujitosa kuwania saini ya nyota huyo.
Madrid wanajiandaa kutuma ofa ya pauni milioni 20 pamoja na mshambuliaji wake wa kimataifa wa Argentina, Gonzalo Higuain, ili kupata saini ya Suarez nyota wa kimataifa wa Uruguay.
Mfaransa anayeinoa Arsenal, Arsene Wenger, amekuwa na mawindo mawili kwa pamoja ya kuwanasa Suarez na Higuain, lakini uamuzi huo wa Madrid unaiweka Gunners katika hatari ya kuwakosa wote kwa pamoja.
Washika Bunduki hao wa London walikuwa na imani kubwa ya kufanikiwa kupata saini ya Suarez kutoka Liverpool, baada ya kuboresha ofa yao kwa nyota huyo na kufikia kitita cha pauni milioni 40.
Gunners ilikuwa ilipandisha dau hilo kutoka ofa ya awali ya pauni milioni 35   zilizokataliwa na kocha Brendan Rodgers, aliyesisitiza kuwa hayuko tayari kumuuza mtikisa mabao wake huyo mwenye umri wa miaka 30 chini ya dau la pauni mil. 55.
Tayari Gunners ilishakubali kumlipa Suarez mshahara wa pauni 120,000 kwa wiki kumng’oa mkali huyo Anfield.
Suarez, hata hivyo, anadaiwa kupendelea kutua Madrid kuliko Arsenal, akiwa na nia ya kukimbia jinamizi la matukio tata dimbani katika soka la England.
Na sasa Madrid inamthaminisha Higuain kwa dau la pauni milioni 35 baada ya kupokea ofa ya thamani hiyo kutoka Napoli, ambapo inajiona iko sahihi kuongeza dau la pauni milioni 20 kukamilisha kitita cha pauni milioni 55 zinazotakiwa na Rodgers.

No comments:

Post a Comment