Saturday, July 20, 2013

Mo Farah
Mo Farah avunja rekodi
BINGWA medali mbili za dhahabu za mashindano ya Olimpiki ya majira ya joto 2012, Mo Farah ameibuka mshindi wa pili wa mbio za Diamond League jijini hapa, huku akivunja rekodi ya mita 1,500 iliyodumu kwa miaka 28 ya mkimbiaji Steve Cram.
Farah, Mwingereza mwenye asili ya Somalia, amejiwekea rekodi ya kuwa mtu wa sita kwa kasi duniani katika umbali huo, baada ya kutumia muda wa dakika tatu na sekunde 28.81, unaomfanya kushikilia rekodi miongoni mwa wakimbiaji barani Ulaya.
Farah, bingwa wa medali za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na 10,000 za Olimpiki ya jijini London mwaka jana, alikuwa wa pili nyuma ya Mkenya Asbel Kiprop, ambaye alikimbia muda rekodi inayoongoza duniani wa dakika 3:27.72.
“Nimeridhishwa na matokeo na kimsingi kulikuwa na ushindani mkubwa katika mchuano huu,” alisema Farah, 30, baba wa watoto wawili pacha.
Cram, aliyekuwa akishikilia rekodi ya dunia, ambaye alitumia muda wa dakika 3:29.67 ambao ni rekodi kwa wakimbiaji raia wa Uingereza iliyodumu tangu Julai 16, 1985, alikiri kushangazwa na kasi ya Farah katika mbio hizo.
Muda huo pia unaingia katika rekodi binafsi za wakimbiaji wa kudumu Sebastian Coe aliyetumia dakika 3:29.77 mwaka 1986 na Steve Ovett (3:30.77) mwaka 1983 ambao walikamata nafasi za pili na tatu miongoni mwa Waingereza kwenye mbio za mita 1,500.

Farah alikuwa katika mbio alizozichukulia kama kipimo binafsi kuelekea mbio za ubingwa wa dunia mwezi ujao jijini Moscow, ambako atakimbia kwenye mbio za mita 5,000 na 10,000. Hakuwa na matarajio yoyote kuweka rekodi ya kutazamwa.

No comments:

Post a Comment