Saturday, July 20, 2013

Wewe ndio mchizi wetu
    Wanachama Simba wanywea kwa Rage
MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, jana aligeuka shujaa kwenye mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na zaidi ya wanachama wapatao 700.
Tofauti na dalili za awali pengine mkutano huo ungekewa na presha kubwa ya wanachama kuhoji mambo mbalimbali ya kiuongozi, mkutano huo jana uligeuka shangwe na nderemo za wanachama kiasi cha kubariki kila walichoelezwa. Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano huo, wanachama wengi walionesha kuridhishwa na utendaji mzima wa kiongozi wao licha ya kuwepo changamoto mbali mbali pia wanastahili kuupongeza uongozi uliopo madarakani chini ya Rage.Baadhi ya wanachama wameomba mabadiliko mbali mbali katika utendaji wa klabu wakiamini klabu hiyo chini ya Rage, watapata mafanikio makubwa katika msimu ujao.Jambo jingine ni wanachama kuombwa kuzika tofauti zilizojitokeza hadi kuibua mgogoro ndani ya klabu hiyo kiasi cha viongozi kujikuta wakigongana wao kwa wao hivyo timu kushindwa kufanya vizuri.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rage alisema hatarajii mapinduzi katika uongozi wake kwani wamekuwa wakichapa kazi kwa mujibu wa katiba  ya klabu hiyo, hivyo msimu ujao utakuwa ni wa mafanikio kwa klabu hiyo.
“Naaamini mambo yatakwenda vizri katika msimu ujao wa ligi na timu itafanya vizuri kutokana na mipango na mikakati tuliyojiwekeza,” alisema Rage na kuongeza wataitisha mkutano mwingine kabla ya Novemba na kuongeza:
“Tunataka tuwe na sera bora za utawala na utendaji ambapo kupitia sera hizi kutakuwa na mfumo bora wa utendaji, kiutawala, kimajukumu na kiuwajibikaji ambapo kila mtu atajikuta anafanya kazi yake,” alisema Rage.
Rage pia amesisitiza msimamo wa kulifuta tawi la Mpira Pesa kwa hoja  wanachama wa tawi hilo wamekuwa wakienda kinyume na taratibu za klabu hiyo wakitaka kuwa juu ya uongozi na kusema jambo hilo halikubaliki kamwe.
“Mpira pesa hawako juu ya Klabu ya Simba, bali ndani ya klabu hiyo, hivyo hatuwezi kuvumilia kuona wanataka kukaa juu ya klabu kitaifa, suala ambalo ni kinyume na utaratibu kabisa,” alisema Rage.
Rage alibainisha kuwa uongozi uliopo madarakani utaendelea kuwajibika katika mambo yote licha ya wanachama hao kutaka kujua hatima ya nafasi ya Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange ‘Kaburu’ akisema nafasi hiyo imezibwa na Joseph Itang’are ‘Kinesi.’
Katika mkutano huo ulidumu kwa dakika 60, agenda zilikuwa kuthibitisha kumbukumbu ya mkutano uliopita, hotuba ya Mwenyekiti na kupokea na kujadili taarifa za kazi kutoka kamati ya utendaji.
Nyingine ni kudhibitisha hesabu za fedha zilizokagaliwa za mwaka uliotangulia, kuthibitisha taarifa za chombo cha ukaguzi na hatua zilizochukuliwa na vyombo
vya utendaji na kudhibitisha bajeti kwa mwaka ujao.
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo majira ya saa 5 asubuhi, ndipo ukumbi ukagubikwa na shangwe za wanachama wakiupngeza uongozi wa klabu hiyo
hadi kumbeba Ragea akionekana ni shujaa.
Hitimisho hilo lilikwenda sambamba na wanachama waliohudhuria mkutano huo, kupewa tiketi ya kuingilia uwanja wa Taifa kujionea mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Simba na URA ya Uganda.
Kuelekea mkutano huo, baadhi ya wanachama walikuwa wakihoji uhalali wa mkutano huo wakidai umeitishwa kinyume cha katiba na wakapanga kwenda mkutanoni kuung’oa. 

No comments:

Post a Comment