Monday, July 29, 2013

Simba wamvutia kasi Oloya
Moses Oloya
KLABU ya Simba inamsubiri kiungo wa kimataifa wa Uganda, Moses Oloya avunje mkataba na Saigon Xuan Than ya Vetinam ili impatie mkataba wa kuitumikia kwa msimu ujao.
Hiyo inakuja siku chache baada ya kuwatimua nyota wanne wa kigeni kutokana na kutorishishwa na viwango vyao ambao ni Mussa Mudde, Assumani Buyinza, Samuel Ssenkoomi, Felix Cuipo na James Kun.
Kutemwa kwa nyota hao, kunaifanya Simba kusaliwa na wageni wawili ambao ni kipa Abel Dhaira na mshambuliaji mpya Amissi Tambwe, raia wa Burundi anayetarajiwa Siku ya Simba (Simba Day) itakayofanyika mwezi ujao.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Pope, wiki iliyopita alizungumza na Oloya na kuahidi atakuja nchini baada ya kuvunja mkataba wake
na Saigon.
“Ijumaa wiki iliyopita, nilizungumza naye (Oloya), akaniambia yuko katika hatua za mwisho kuvunja mkataba wake, baada ya kufanikiwa hilo atakuja kusaini rasmi Simba,” alisema na kuongeza kuwa msimu huu wameamua kufanya usajili kwa utulivu mkubwa.
Pope alisema kama watafanikiwa kupata saini kiungo huyo, wanaimani msimu ujao watakuwa na kikosi imara hivyo kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu kutokana na uwezo wa mchezaji huyo.
Alisema hata kama itatokea wakamkosa nyota huyo kwa ajili ya raundi ya kwanza ya ligi hiyo itakayoanza Agosti 24, watahakikisha wanafanikisha wanakuwa naye katika raundi ya pili kutokana na mchezaji huyo kukubali kutua Msimbazi.
Oloya, kiungo alitezaliwa Oktoba 22, mwaka 1992, kabla ya kutimkia Vietnam, msimu wa 2009/10 aliichezea KCC ya Uganda kabla ya kutua Saigon mwaka 2011 na kuichezea mechi 29 hadi sasa, akifunga mabao matano. Ameichezea Uganda mechi 22.

No comments:

Post a Comment