Monday, July 29, 2013

Dortmund yamkaribisha rasmi Guardiola
PEP Guardiola juzi usiku alijikuta akiandika historia ya kuchapwa katika mechi ya kwanza ya kimashindano klabuni Allianz Arena, baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-2 kutoka kwa Borussia Dortmund na kutwaa ubingwa wa Supercup.
Bayern Munich, ambayo iliichapa Dortmund katika fainali ya Mabingwa Ulaya Mei mwaka huu kwenye dimba la Wembley jijini London, ilishindwa kumzuia Marco Reus kufunga mara mbili na kuipa Dortmund ubingwa ndani ya Uwanja wa Westfalenstadion.
Wakati Bayern ikishindwa kurejea ilichofanya katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mholanzi Arjen Robben – ambaye alifunga bao la ushindi Wembley, alimudu kurejea hilo kwa kufunga mabao yote mawili juzi.
Akizungumzia pambano hilo baada ya filimbi ya mwisho, Guardiola alisema: "Ingawa tumepoteza pambano hili, bado sihisi kuwa Dortmund walikuwa bora kuliko sisi.
"Tuna siku 10 kabla ya ufunguzi wa msimu wa Bundesliga, hivyo tuna muda wa kusahihisha makosa madogo madogo yaliyotugharimu katika mechi hii," aliongeza Guardiola.
Guardiola, ambaye alitwaa jumla ya mataji 13 katika miaka yake minne ya kuinoa FC Barcelona aliyoiacha mwaka jana, ana kibarua kigumu kudumisha makali yaliyoachwa na kocha aliyechukua nafasi yake Jupp Heynckes klabuni hapo.
Chini ya Heynckes, Bayern iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Ujerumani kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ‘Bundesliga,’ Mabingwa Ulaya na Kombe la Ujeruman (DFP Pokal), iliyotwaa msimu uliopita.
Bayern ambayo ilicheza bila nyota wake Franck Ribery na Bastian Schweinsteiger, huku ikimkosa pia Mario Gotze – aliyetua hapo akitokea Dortmund, hiki ni kipigo chake cha kwanza wakati huu wa maandalizi kuelekea msimu mpya.
Kabla ya hapo, Bayern ilizichapa Fanclub Wildenau mabao 15-1, TSV Regen 9-1, Paulaner Dream Team 13-0, Brescia 3-0, Sonnehof Grossapac 6-0, Hansa Rostock 4-0, Hamburg 4-0, Borussia Monchengladbach 5-1, kabla ya kuichapa Barcelona mabao 2-0.
Kwa upande wake kocha wa Dortmund, Jurgen Klopp alisema: "Ilikuwa ni mechi kubwa, timu zote zikipanda kushambulia na kujilinda vema, kana kwamba hakuna kesho.
“Jambo la msingi ni kuwa Bayern sio wapinzani wetu pekee, tumejibidisha kama sisi.”
Bayern inatarajia kufungua msimu wa Bundesliga kwa kuwavaa Borussia Monchengladbach Ijumaa ya Agosti 9, wakati Dortmund itaumana na Augsburg siku baadaye.

No comments:

Post a Comment