Monday, July 29, 2013

Mourinho: Wenger ni mchizi wangu
MAKOCHA wa klabu hasimu za Arsenal na Chelsea, Arsene Wenger na Jose Mourinho, kwa sasa ni kama maswahiba wakubwa, ambapo Mourinho amekiri kuwa anamheshimu mno Wenger licha ya klabu zao kuwa pinzani.
Ukaribu wa Wenger na Mourinho, umeonekana kwa wawili hao kuambatana pamoja wakati wa chakula cha usiku nje ya makazi yao, ambapo Special One amesisitiza kuwa heshima yake kwa Wenger inatokana na mafanikio yaliyotukuka akiwa Arsenal.
Mourinho raia wa Ureno, alisema: “Yeye ni mtu mzuri sana. Namheshimu sana yeye na daima natarajia kuonyesha heshima zaidi kwake.
“Nisingependa kuwa na tatizo lolote baina yetu. Wakati unapokuwa huko katika ligi hiyo na wakati kunapokuwa hakuna mechi baina yetu, ni rahisi mno kuwajua watu.
“Na mimi nilikuwa na nafasi bora zaidi ya kukutana na yeye wakati nilipoondoka England, katika UEFA, michuano ya Euro, Kombe la Dunia. Tulikutana katika chakula cha jioni na ilikuwa ni nyakati nzuri. Nilikuwa nafurahia kuzungumzia soka na yeye.”
Mourinho alienda mbali zaidi na kufichua kuwa yeye anaweza kujifunza kutoka kwa Wenger, namna sahihi ya kudumu na klabu moja kwa zaidi ya miaka mitatu.
Mreno huyo alisema: “Wenger ananifundisha mimi namna gani ya kudumu hapa kwa miaka 17. Hilo lilikuwa moja agenda wakati wa mazungumzo yetu ya mwisho.
“Kupewa na kupata heshima kama anayopata kutoka kwa bodi ya klabu ni jambo muhimu. Sio kutokana na uso wake nzuri, bali ni kutokana na kazi bomba aliyofanya.
“Alikuwa na nafasi nyingi tu za kutimka Gunners, yote ni kutokana na nia nzuri ya klabu kwake, hivyo wakati akikataa ofa za kuhama na kutaka kubaki Emirates ni kwa sababu anapapenda na sababu ikiwa ni matarajio yake ya baadaye,” alimaliza Mourinho.

No comments:

Post a Comment