Monday, July 29, 2013

Madrid yamvalia njuga Bale
Gareth Bale
MIAMBA ya soka la hapa, Real Madrid, juzi usiku ilipiga hatua inayotajwa kuweza kuwa ya mwisho katika jitihada zake za kupata saini ya winga Gareth Bale wa Tottenham kwa ofa inayofikia thamani ya pauni milioni 95 ikihusisha pesa na wachezaji wawili.
Madrid imeripotiwa kuwa iko tayari kutoa kitita cha pauni milioni 51, sambamba na wachezaji wawili, Angel Di Maria anayethaminishwa kwa dau la pauni milioni 25 na Fabio Coentrao pauni milioni 19 – kufanikisha ililoliita ‘dili la karne.’
Tayari Madrid ilishatoa ofa rekodi ya dunia ya pauni milioni 81 kuomba ridhaa ya kumnasa winga huyo wa kimataifa wa Wales, ambalo lilikataliwa na Spurs na kumshangaza hata mchezaji husika.
Lakini, Rais wa Madrid, Florentino Perez, ameenda mbali zaidi katika ofa mpya ya kujaribu kumfanya Bale kuwa nyota mpya wa The Galactico.
Ofa hii mpya ya Madrid, inatabiriwa kumsukuma Mwenyekiti wa Tottenham, Daniel Levy, ambaye amekuwa mbali, asiyetaka kujadili suala hilo, kuridhia uhamisho huo.
Bale juzi alipaza sauti kumwambia Levy kuwa anahitaji ridhaa ya kwenda kujiunga Madrid, huku akimkumbusha mwenyekiti huyo kukumbuka ahadi kuwa angemruhusu kuhama kama klabu hiyo ya White Hart Lane ingekosa tiketi ya mabingwa Ulaya.
Licha ya kumuomba mwenyekiti kubariki uhamisho wake, Bale, 24, amekana mbinu chafu ya kuishinikiza Spurs kumuuza.
Kocha wa Tottenham, Andre Villas-Boas, anatambulika alivyo shabiki wa winga wa kimataifa wa Argentina, Di Maria, 25 ambaye anaambatanishwa katika jaribio la sasa la Madrid.
Na haitarajiwi kama anaweza kukana kuungana na Mreno mwenzake Coentrao, 25, ambaye anaweza kutumika kama beki/winga wa kushoto - mzalishaji wa mashambulizi ya pembeni kutokea nyuma.

No comments:

Post a Comment