Saturday, July 27, 2013

Wamiliki wakana kuiuza Liverpool
KAMPUNI ya Fenway Sports Group (FSG) imezikana taarifa za vyombo vya habari zilizodai kuwa inajiandaa kuiuza klabu ya Liverpool.
Magazeti yaliripoti Ijumaa, mabilionea wawili raia wa Marekani na kampuni moja ya Saudia inayojihusisha na uuzaji wa mafuta, zimeingia katika mazungumzo ya kuinunua Liverpool kutoka kwa FSG, ambayo ilidaiwa kutaka dau la pauni milioni 350.
Kutokana na taarifa hizo, kwa pamoja FSG na Liverpool zimekanusha kwa nguvu moja habari hizo na wamiliki wa Kimarekani ambao walianza kuimiliki Liverpool tangu Oktoba 2010, walielezea nia yao ya kuendelea kubaki Anfield.
Msemaji wa Fenway Sports Group alisema: “Kama ulivyowahi kuwa uvumi mwingine wowote kuhusu kuuzwa kwa Liverpool Football Club, hakuna ukweli wowote pia katika tetesi hizi.
“Hatujawahi kuwa na mkutano na mtu yeyote kuhusu kuiuza klabu, hatujui ni nani hasa chanzo cha uvumi huo, na lolote linalohusiana na upotoshaji juu ya mauzo ya Liverpool.”
Naye msemaji wa Liverpool, akaongeza: “Fenway Sports Group imeweka wazi kila kitu Liverpool Football Club haiuzwi. Hakuna ukweli wowote katika habari hiyo.”

No comments:

Post a Comment