Friday, July 26, 2013

Stars yaapa kufia Uganda
Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa katika mazoezi yao ya mwisho kabla ya mechi na Uganda
WAKATI timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars inashuka dimbani leo kuwakabili Uganda Cranes katika mechi ya kuamua tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwa fainali za Afrika kwa nyota wa ndani (CHAN) hapo mwakani, Kocha 
Kim Poulsen amesema kazi kubwa kwa vijana wake ni kupambana mwanzo mwisho kupata mabao ya mapema.
Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya bia kupitia kinywaji chake cha Kilimanajro Premium Lager, inawakabili Uganda ikiwa nyuma kwa bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya kwanza baina yao iliyochezwa Julai 13, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Kampala jana kuhusu kikosi chake, Poulsen alisema vijana amejiandaa vizuri na kwamba licha ya kuwa ni mwezi mgumu kisoka kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa kwenye mfungo, wachezaji wamepania kupata matokeo mazuri.
“Tunajua watanzania wengi walikataa tamaa au kupoteza matumanini baada ya sisi kufungwa 1-0, lakini katika mpira haya yanaweza kubadilika…tukifunga bao kesho litabadilisha kila kitu,” alisema Poulsen.
Alikiri kuwa mechi hii ya marudiano ni ngumu kwani Stars itakuwa inacheza na timu bora Afrika Mashariki
lakini lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90 au zaidi za mchezo.
Alisema licha ya kuwakosa wachezaji Shomari Kapombe na Mwinyi Kazimoto, maandalizi ni mazuri na hasa walipokuwa kambini Mwanza wachezaji walionesha bidii sana katika mazoezi.
Alisema katika mechi ya kesho watajitahidi kutengeneza nafasi nyingi na kufunga magoli. “Katika mazoezi yetu tumefanya mazoezi sana katika ushambuliaji, kutengeneza nafasi na kufunga magoli,”alisema huku akiongeza kuwa mabeki watahakikisha washambuliaji wa The Cranes hawapiti kabisa.
Aliwataka watanzania wawe na imani na timu ya Taifa kwa matokeo yoyote yatakayopatikana kesho kwani mpira ni safari na kukubali matokeo ni sehemu ya mchezo.
“Wachezaji wana ari ya kupata ushindi ili waende CHAN mwakani kwani hii itawapa nafasi nzuri ya kuonekana na vilabu kubwa duniani na tayari tumeona jinsi watu wengi wametambua kuwa kuna wachezaji wazuri Tanzania….Kapombe ameenda kwenye majaribio Uholanzi, Kyemba naye yuko njiani na nasikia Kazimoto yuko Qatar..nawatakia kila la heri.” Alisema.
Poulsen alisema Jumatatu atazungumza na waandishi wa habari kuhusu mipango ya muda mrefu ya Taifa Stars.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye Bia yake inadhamini Taifa Stars alisema wao kama wadhamini wanawaomba watanzania wawe na imani na stars na waiombee ifuzu mashindano ya CHAN.
“Sisi kama wadhamini tuna imani na timu yetu na tuna imani watafanya maajabu katika mechi ya kesho ili wawape raha watanzania,” alisema Kavishe.
Kilimanjaro Premium Lager imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2 kwa mwaka kuidhamini timu ya Taifa kwa mkataba wa miaka mitano.
Cranes inawakabili Stars leo ikiwa na tatizo la ufungaji kwani katika mechi mbili za kirafiki ilizocheza na vijana wa chini ya miaka 23 na kufungwa zote kwa bao 1-0 ambazo Denis Iguma aliyewafungia bao Julai 13, alichezeshwa sehemu ya kiungo.
Micho atawakosa wachezaji wake wawili wa mbele,  Tony Odur na Patrick Edema. Wakati Odur anauguza nyonga, Edema amekwenda Ureno kwa majaribio.
Katika kuziba pengo, Micho amewaita Simon Okwi (KCC FC), David Kasirye (URA FC) na Henry Oguti anayechezea Kiira Young.
Hata hivyo, Okwi ameitwa licha ya kushindwa kufungia bao KCC msimu uliopita huku kukiwa na shaka juu ya kiwango cha Kasirye.
Mazingira hayo yanamfanya Micho amtegemee Oguti kuongoza safu ya ushambuliaji anayeonekana kuwa na nguvu kuliko wengine ingawa kuna mwingine kama Frank Kalanda.

No comments:

Post a Comment