Friday, July 19, 2013

Alvaro Negredo
Negredo atua Man City kwa rekodi Sevilla
MANCHESTER City imefanikiwa kumsajili Alvaro Negredo kwa kitita cha pauni mil 24 kutoka Sevilla ya Hispania kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania, ametua Manchester City akiwa mchezaji wa tatu kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao huku ikikaribia kumnasa pia  mshambuliaji wa Fiorentina,
Stevan Jovetic.
Wakati ikicheua pauni mil 24 kumpata Negredo, inaweza kumpata Jovetic kwa kiasi cha pauni mil 23, hivyo hadi sasa imetumia jumla ya pauni mil 90 kwa usajili.
Tayari Negredo (27), ameshafanyiwa vipimo tangu Alhamisi kabla ya kujiunga rasmi na Manchester City iliyomaliza ziara yake nchini Afrika Kusini tangu juzi ikifungwa 2-1 dhidi ya AmaZule.
Negredo ni kati ya washambuliaji wazuri kwani katika msimu uliopita, alimaliza nafasi ya nne kwenye La Liga kwa kufunga mabao 25, nyuma ya Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Radamel Falcao.
Nyota huyo aliyeweka rekodi ya usajili kwa klabu yake ya Sevilla, ameondoka baada ya kuitumikia kwa misimu minne akiifungia mabao 70.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Hispania, amecheza mechi 14 na kuifungia mabao sita.
Akizungumzia kuhama kwake, Negredo alisema miaka yake mine ya kucheza Sevilla ilikuwa ya furaha kubwa, lakini wakati wa kucheza hapo, umekwisha anafurahia kujiunga na timu kubwa.
Negredo ni kama amemfuata nyota mwingine wa zamani wa  Sevilla, Jesus Navas aliyetua Etihad mwezi uliopita pamoja na kiungo mwingine Mbrazil Fernandinho.
Negredo atakuwa akivalia jezi namba tisa ambayo ilikuwa haina mtu tangu aondoke  Emmanuel Adebayor, nyota wa kimataifa wa Togo.

No comments:

Post a Comment