Thursday, July 25, 2013

Azam kukipiga na 'vigogo' Sauzi
Wachezaji wa Azam FC wakishangilia moja ya mechi zao
KLABU inayokuja kwa kasi katika medani ya soka hapa nchini, Azam FC, inatarajiwa kucheza mechi nne za kirafiki katika ziara yao nchini Arika Kusini ikiwamo dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, Orando Pirates.
Azam FC, klabu inayozipa changamoto klabu kongwe za Simba na Yanga kutokana na uimara wake kila idara, tofauti na wakongwe hao wanaojiendesha kwa kuunga kuunga.
Meneja wa Azam FC, Said Jemedari, alisema kila kitu hadi sasa kinakwenda sawa na inasubiriwa siku ya kukwea pipa kwenda kufanya ziara yao, ambayo itakuwa na manufaa kwa timu nzima ambayo inakabiliwa na michuano mbalimbali hapo mbeleni.
Jemedari alizitaja timu ambazo wataumana nazo katika ziara yao ya siku 12 kuwa ni Amazulu, Supersport United, Bidvpst Wits pamoja na Orando.
“Tuna imani mechi hizo nne zitamuonyesha mwalimu wapi tuendako na kujua makosa ya kufanyia maboresho kabla ya mchezo wetu na Yanga Agosti 17 na Ligi Kuu,” alisema Jemedari.
Katika hatua nyingine, Jemedari alisema juzi walishuka dimbani kumenyana na Kombaini ya Majeshi, mchezo uliopigwa dimba la Chamazi nje kidogo ya jiji na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, mabao yalifungwa na Hussein Nyamandulu wa CISM na Tchetche Kipre kwa Azam FC.
CISM inaundwa na wachezaji wa timu za Jeshi ambazo ni JKT Ruvu, Mgambo, Ruvu Shooting, Oljoro, Trans Camp, Kipanga na Rhino Rangers ipo katika maandalizi ya kushiriki mashindano hayo yatakayorindima kuanzia timu za Majeshi Afrika Mashariki yatakayofanyika Agosti 5-17 jijini Nairobi nchini Kenya.

No comments:

Post a Comment