Friday, July 19, 2013

Luis Suarez
Arsenal yampandia dau Luis Suarez
KLABU ya Arsenal imezidi kuonesha nia yake ya kupata saini ya mshambuliaji mtukutu Luis Suarez, raia wa Uruguay baada ya kuongeza dau hadi pauni mil 40 ili aweze kutua Emirates.   
Kiasi hicho ni nyongeza ya pauni mil 5 ya dau la awali la pauni mil 35 ambalo lilitupwa na Liverpool licha ya nyota huyo kuonesha wazi kutaka kuhama Anfield na kwenda Arsenal.
Habari zinasema, kwa kiasi hicho kipya cha fedha huenda suala la mchezaji huyo likapata ufumbuzi ndani ya saa 48 kuanzia jana kwani tayari Kocha Arsene Wenger anajiandaa kuwasilisha ofa hiyo mpya.
Kuna habari kuwa, Arsenal sasa imeamua kuacha mambo mengine ili kupigania usajili wa nyota aweze kucheza Emirates msimu ujao.
Wakati Arsenal ikipambana kusaka saini ya nyota huyo, Liverpool nayo imekuwa ikijitahidi kumzuia asiondoke kutokana na umuhimu wake dimbani.
Mbali ya Arsenal, Suarez amekuwa akimezewa mate na klabu kadhaa ikiwemo Real Madrid ya Hispania
Pamoja na Arsenal ‘kujikamua’ hadi kiasi cha pauni mil 40, Kocha wa Liverepool,  Brendan Rodgers amekuwa akisema thamani ya nyota huyo ni pauni mil 55 kama ya Edinson Cavani.
Cavani ambaye pia ni nyota wa kimataifa wa Uruguay, amejiunga na Paris Saint-Germain tangu Jumanne wiki hii akitokea Napoli ya Italia.
Pamoja na kauli ya kocha huyo, hatima ya mchezaji huyo atakayekosa mechi sita za awali za Ligi Kkuu, itaamuliwa na mmiliki wa klabu hiyo,
Kampuni ya Fenway Sports Group ya Marekani inayomiliki klabu hiyo.
Kuna uwezekano wa Arsenal kufanikiwa mpango huo kutokana mkataba wake kuonesha kuwa hiyo ndio 
thamani yake ya kuuzwa.
Lakini, Liverpool imedai kuwa suala la thamani hiyo kuandikwa kwenye mkataba, haina maana ndio tahamni halisi ya nyota huyo kuondoka Anfield.
Hata hivyo, Arsenal inaamini kuwa itampata mchezaji huyo ambaye amekuwa na shauku ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wakati hayo yakiendelea, Suarez anatarajiwa kujiunga na Liverpool hapo kesho kwa safari ya kwenda
Australia kwa ziara ya mechi za kirafiki kwa ajili ya msimu ujao.
Suarez ni chaguo la kwanza la Wenger katika msimu huu kabla ya kuangalia uwezekano wa kuwapata Gonzalo Higuain wa Real Madrid ya Hispania na Wayne Rooney wa Manchester United.
Kuhusu Higuain, nyota wa kimataifa wa Argentina, Real Madrid imeshasema kwamba inataka kiasi cha pauni mil 25.5 ili kumruhusu.

No comments:

Post a Comment