Friday, July 26, 2013

Ahly, Zamalek zatoka sare 1-1
KIUNGO Mohamed Aboutrika wa Ahly, Jumatano usiku aliifungia bao timu yake kwa mkwaju wa penalti na kuisaidia kuvuna sare ya bao 1-1 dhidi ya Zamalek katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Ingawa baadhi ya mechi za makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho zilichezwa mwishoni mwa wiki, mechi ya timu hizo mbili ilisogezwa hadi Jumatano kutokana na vurugu zilizoukumba mji wa Cairo na Alexandria.
Aboutreika alifunga bao kwa penalti dakika 27 kabla ya filimbi ya mwisho baada ya Salah Soliman wa Zamalek kumchezea vibaya mshambuliaji Ahmed Abdel-Zaher.
Bao hilo lilirejesha furaha kubwa wapenzi na mashabiki wa Ahly kutokana na timu yao kuwa nyuma tangu dakika ya nane baada ya Ahmed Gaafar kuifungia timu yake bao, akimtungua kipa Sherif Ekramy.
Kwa sare hiyo, timu zote za kundi A, zimelingana kwa pointi moja kwani katika mechi ya mwishoni mwa wiki, timu za Orlando Pirates ya Afrika Kusini na AC Leopards ya DR Congo zilishindwa kufungana.
Mechi hiyo ya Zamalek na Ahly, ilichezwa mjini El Gouna, badala ya Cairo kutokana na sababu za kiusalama baada ya uwepo wa maandamano ya wafuasi wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Morsi.
Ingawa awali mechi hiyo ilitakiwa ipigwe bila mashabiki, lakini kutokana na ulinzi mkali wa vyombo vya usalama, mashabiki wapatao 7,000 waliingia kwenye uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 12,000.
Matokeo hayo yanaifanya Ahly kuongoza kundi A, ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na wapinzani wakubwa katika ligi ya Misri, Zamalek pia wenye poiinti moja kama ilivyo kwa Leopards ya DR Congo na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Libolo FC ya Angola inaongoza kundi B, ikiwa na pointi moja ikifuatiwa na Coton Sport ya Cameroon, Sewe ambazo hazijacheza na Esperance ya Tunisia iliyopoteza mechi ya kwanza mjini Luanda.

No comments:

Post a Comment